SHEIKH NDUNGO ASHINDWA KUMZIKA BABA YAKE MZAZI
Na Kombo Hassan
Ijumaa,30/09/2016
Mtihani juu ya mtihani imeendelea kuwafika ndugu zetu katika imani ya Dini ya Uislamu, wanaotuhumiwa kwa tuhuma mbalimbali za Kesi za Ugaidi, kwa mtu mmoja baada ya mwingine ndani na nje ya magereza wanayoendelea kushikiliwa. Sheikh, Ndungo Nasir, ambaye ni baba wa familia, anayeendelea kusota mahabusu kwenye Gereza la Maweni, Tanga, akikabiliwa na tuhuma za “Ugaidi” na kufunguliwa kesi ya uchochezi, mapema wiki iliyopita, ameshindwa kuhudhuria mazishi ya baba yake mzazi Mzee Nasir, aliyefariki nyumbani kwa mtoto huyo wa pekee aliyekuwa akimuuguza kwa muda mrefu, Mjini Tanga, kabla ya kukamatwa kwake. Na mwili wake ulisafirishwa kwenda kuzikwa kwenye Maziara yao kwenye Kijiji cha Tawalani, Wilaya ya Mkinga, Tanga. Sheikh Ndungo, ambaye ni Imamu wa Msikiti na “Daiyah” alikamatwa mapema mwaka huu mnamo Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, wakati wa Magharibi akifuturu yeye na familia yake nyumbani kwake katika Maeneo ya Sahare, Tanga. Kuendelea kushikiliwa kwa Sheikh, Ndungo, kwenye mazishi ya baba yake mzazi kulidhihirisha ni jinsi gani familia yake ilivyopatwa na pigo au msiba mzito wa yeye kuendelea kushikiliwa mahabusu, kwani watu wengi walidhihirika kumlilia na kumsikitikia yeye zaidi kuliko hata baba yake aliyefariki, kwani yeye kabla ya kukamatwa kwake alikuwa ni muhimili mkubwa mno wa familia yake kiuchumi, kimalezi, kielimu, kidini, n.k. Na baadhi ya ndugu wa Familia ya Sheikh Ndungo, katika kuonyesha huzuni yaliyonayo juu yake, mnamo Jumapili ya wiki iliyopita waliongozana kwenda katika Gereza la Maweni, kwa ajili ya kwenda kumjulia hali na kumpa “Mkono wa Tanzia” kwa ajili ya kumtakia subira na kumuombea kila la kheri kwa Fitina ya Mtihani aliyokadiriwa na Allah (Aliye Mtukufu) kumfika kwa hekima yake. Wakati, huo huo katika kadhia inayoendelea ya kamatakama ya Waislamu, mjini Tanga, wanaotuhumiwa kwa tuhuma za “Uchochezi na Ugaidi”, miongoni mwao ambao waliopatwa na fitina ya mtihani huo ni Sheikh Ali Kiroboto, Mudir wa Maahad Daarul-Ulum, Waalimu wawili wa Somo la Maarifa ya Uislamu, katika mashule mbalimbali ya sekondari na Wahadhiri wa Dini ya Uislamu, ndani ya Jiji la Tanga, Masheikh, hao pia wamesema wamepewa namba za kuripoti, na ni Sheikh Chambuso Ramadhani, na Sheikh Hamad Ayubu Kidege, na waliripoti Ijumaa iliyopita ikiwa ni mara yao ya nne tangu kukamatwa kwao na kutakiwa kusaini kila siku ya Ijumaa, kwenye idara ya Polisi ya Upelelezi, Mjini Tanga, wakitokea majumbani mwao baada ya kuachiwa kwa dhamana. Na ni kwamba simu zao mpaka ikiandikwa makala hii, bado zilikuwa zipo mikononi mwa Polisi zikifanyiwa uchunguzi wa kipelelezi, kwa nyakati tofauti walisema Masheikh hao. Pia alihoji Sheikh, Kidege: “Mbona inaonekana tunaoripoti ni Waislamu pekee yetu tu? Je, wenye tuhuma za Ugaidi na Uchochezi Hapa nchini ni Waislamu tu?” alisema Sheikh Kidege. Hii ndio hali inayoendelea na kuwakabili Waislamu kwa sasa Tanzania hususani Tanga. Wabillah Tawfiq.