Tujitahidi kusema Ukweli uliotafitiwa

Na Alhuda,Alkhamis 27 Novemba 2014
Wakati jamii ya Waingereza ikiwa na msemo, ‘no research, no right to speak,’ jamii ya Waislamu ina utajiri mkubwa zaidi wa kanuni za kuchunga kauli.
Qur’an inaonya kuwa viungo vyote vitaulizwa ikiwa ni pamoja na mdomo. Hadith ya Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, inasema, kukaa kimya ni bora kama hakuna la kusema. Haya ni mafunzo yanayojenga nidhamu adhimu ya mazungumzo.
 
Mtu anayezungumza jambo analolijua huwa katika nafasi nzuri ya kuuweka ukweli mahali pake sahihi. Lakini mtu anayezungumza jambo asilolijua huwa katika hatari kubwa ya kuutoa ukweli mahali pake na kukaribisha urongo.
 
Madhara ya kusema jambo pasipo kulijua ni mengi. Kitendo hicho kinaweza kumgharimu msemaji mwenyewe, au kinaweza kumgharimu mwingine au kuigharibu hata jamii.
 
Huwa ni baada ya gharama kubwa kuweza kuurudisha ukweli mahali pake. Matatizo mengi yanayotokea huwa ni matokeo ya kuundosha ukweli mahali pake. Dhana ya haki, kwa kiasi kikubwa, inabebwa na nafasi sahihi ya ukweli.
 
Hakuna binadamu anayeupenda uongo japo wengi huongopa au kudanganya. Tabia ya kusema jambo bila uhakika ina asilimia kubwa ya khulka ya uongo. Yeyote anayejaribu kulisemea jambo pasipo uhakika anajenga ujasiri mbaya wa kusema uongo.
 
Na yeyote anayekataa kulisemea jambo asilolijua hujenga nidhamu ya kusema ukweli. Moyo wenye khofu ya kusema jambo usilolijua ni moyo unaojiweka jirani na ukweli.
Lakini moyo wenye uthubutu wa kusema usilolijua ni moyo unaojiweka karibu zaidi na uongo. Kusema kweli, maisha ya jamii zetu yameupa nafasi kubwa zaidi uongo.
 
Tabia hasi ya kusema mambo pasipo uhakika au kuujua undani wake halisi imeshamiri kwa sura mbalimbali. Imefika mahali mtu huthubutu hata kumuelezea mtu au kutoa taarifa zake pasipo kumjua wala kukutana naye.
 
Tabia hiyo imeikumba hata tasnia ya uandishi ambapo mwandishi hudiriki kulisemea jambo pasipo uhakika. Ni taarifa za mezani zaidi kuliko utafiti zinazojaza kurasa na hata kubebwa na vichwa vikubwa wakati mwingine kwa malengo ya kibiashara.
 
Kwa muumini kuna kinga mbili za kumnusuru na tabia hiyo. Kwanza ni imani ya kumkhofu Mwenyezi Mungu, na kuikhofu Siku ya Mwisho ambapo ukweli wa mambo yote utabainishwa.
 
Kinga ya pili ni matumizi sahihi ya akili. Akili ikitumika vizuri huwa na uwezo wa kutafakari mara nyingi kabla ya kusema au kuamua. Watu hufikiri kwanza kabla ya kusema.
 
Wakati Imani ina matokeo mema Akhera, akili nayo pia ina daraja kubwa Akhera. Kuna Hadith inayosema, “Watu walimsifu mtu mmoja mbele ya Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, kwa uzuri sana na kumsema kwa mambo yote mazuri. Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, akawauliza: Mtu huyo ana akili kiasi gani?”
 
Wakamjibu: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Sisi tunakueleza yanayomuhusu (mtu huyo) kulingana na bidii katika ibada na kheri nyinginezo, nawe unatuuliza kuhusu akili yake!” 
 
Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, akawajibu: “Mpumbavu hupatwa na makubwa kwa upumbavu wake kuliko machafu ya mchafu (wa vitendo). Na kesho watu watapanda daraja kubwa na kuwa karibu na Mola wao kwa kadiri ya akili zao.”
 
Hadith hiyo inatubainishia nafasi ya akili. Akili ina uwezo wa  kumzuia mtu  kufanya jambo ambalo haikubaliani nalo. Ni dhahiri kuwa kusema jambo ambalo mtu hana uhakika nalo kunakinzana na akili.
 
Akili huwa na kasumba ya kutaka kutoshelezwa kabla ya kuruhusu uamuzi. Lakini akili inapojua kuwa haijui chochote kuhusu jambo fulani huwa haikubali jambo hilo litoke kwenye kinywa cha mwenye akili hiyo.
 
Lakini kwa vile nafsi ina nguvu ya kufanya maamuzi hata kama yanapingana na akili, basi mtu hujikuta akifanya jambo linaloweza kumletea madhara pengine kuliko hata yale anayoyapa mtu mchafu wa vitendo.
 
Licha ya matendo yake mema, mtu mwema anaweza kujikuta katika majuto makubwa kwa sababu ya kushindwa kutumia akili. Tunasisitiza kuwa imani na akili viwe kinga ya Muumnini katika kauli. Tunyamaze kama alivyotunasihi Mtume, au tuseme ukweli uliotafitiwa.

Matangazo maalum ya kibiashara (nafasi hii inalipiwa)

زيت ارغان    Mafuta ya Arghani mafutayaarghani

Matoleo mapya ya kitabu kipendwacho cha Mkweli Mwaminifu yako tayari.Agizia mapema kutoka kwetu.

mkweli mwaminifu 

Suruali za kuvalia kanzu za kiume. na za kike

Zipo za ukubwa na rangi mbali mbali .Ni mali kutoka nchini Morocco.

Zinapatikana Kwa reja reja na kwa jumla .Ili Kujua zaidi wasiliana nasi hapa.

 

  SURUALI MOROCO      SURUALI MOROCCO

MWANGAZA KWA UMMA

Tofauti kati ya Tohara na kukeketa
Na Skh Mussa Kileo

Kila inapofika tarehe 6 Februari, Umoja wa Mataifa huadhimsha siku ya kupinga ukeketaji wa wanawake Duniani . Kwa wanaharakati wa Haki za binaadam na jinsia huiadhimisha siku hii kwa kauli mbiu mbalimbali na maazimio ya kushinikisha jamii ibadilike ili iachane na kuwakeketa wanawake.

Ukeketaji ni jambo lilioenea katika vinywa vya watu na kuandikwa na asasi mbali mbali za kijamii,na ipo haja kubwa kwa jamii ya kiislaam kulichambua jambo hili kwa kina,na ufafanuzi kama ifuatavyo:

Endelea