Vita Syria: Je, Ni Suni Vs Shia? Ipi Nafasi ya Ummah?

Makundi ya Nje ya Syria yamekosea Kuingilia kivita!
Na S. Hussein

 Ulimwengu wa Waislamu una mtihani mkubwa chambilecho Mhariri wa gazeti hili katika maoni yake ya toleo lililopita. Siku mbili tu baada ya maoni hayo, nilishuhudia maandamano makubwa ya Waislamu nchini Misri ambapo Rais wa nchi hiyo, Mohammed Mursi, aliwahutubia Masheikh na Waislamu wengine wa nchi hiyo, na kutangaza rasmi kufunga mpaka wa nchi yake na Syria.

 Aidha, Mursi aliyataka makundi yaliyojiingiza katika vita hivyo kutoka nje ya mipaka ya Syria yaondoke mara moja. Bila kuficha alilitaja wazi kundi la Hisbullah la Lebanon ambalo limeingia nchini Syria kumsaidia Rais Asad kwa misingi ya Kimadhebu.

Wachambuzi wengi wa Kiislamu waliikwepa mada ya Syria kwa sababu amabazo kweli zimejitokeza hivi sasa. Walikwepa kuzielekeza kalamu zao upande wa serikali na upande wa Wapinzani wake walioshika silaha.

Walichochelea waandishi hawa ni kwamba wangeweza kujitokeza upande fulani mwanzoni, halafu baadae mambo yangebadilika na kuzilazimu kalamu zao kubadili maelezo.

Tofauti na vuguvugu la mabadiliko kwa njia ya mapinduzi ya umma katika nchi za Tunisia na Misri ambako suala la madhehebu halikuwa na nafasi, Vita vya  Syria vilishakuwa na dalili ya mgawanyiko wa kimadhehebu tangu mwanzo. Jamii ya Wasyria ina mseto wa Waislamu wa Kishia na Kisuni.

Misimamo ya Mataifa ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na Saud Arabia, Misri, Uturuki ilishabainika kitambo kuwa dhidi ya serikali ya Asad. Hata hivyo, hakukuwa na harakati za wazi za kijeshi za Mataifa hayo ukiacha matamko ya kumtaka Rais Asad apishe mabadiliko.

Japo kulikuwa na tetesi za wanamgambo kupatiwa misaada ya kijeshi kutoka nje lakini hilo halikuwa na ushahidi wa moja kwa moja. Kusema kweli haikusikika sauti ya Mataifa hayo ya mlengo wa Suni kujiingiza katika mapambano hayo kijeshi.

Hii ilikuwa ni nafuu kubwa kwa Waislamu ulimwenguni kote, na, kwa kweli, hakukuwa na hamasa ya makundi ya Waislamu ulimwenguni kuunga mkono upande wowote ule. Wengi wao waliamini kuwa ni upepo tu wa mageuzi uliowahusu Wasyria wenyewe.

Lakini hatua ya makundi ya mlengo wa Kishia kujiingiza moja kwa moja katika vita hiyo imechochea hamasa mpya kutoka ile ya upepo wa mageuzi ya Wasyria kuja mapambano ya kimadhehebu.

Maandamano niliyotangulia kuyataja ya Misri, yenyewe pia, yalitokana na hamasa hiyo ya kutaka nchi yao isiikalie kimya hatua ya kundi la Hisbullah la Mashia kujiingiza nchini Syria.

Baada ya Misri kujitokeza hivyo, bila shaka, picha sasa imeonekana wazi kuwa Syria kunafuka moshi kama si kuwaka moto wa madhehebu. Na huu ni ugomvi wa hatari zaidi ambao utaugawa ulimwengu wa Waislamu, Suni upande wao, na Shia upande wao.

Tayari kulishakuwa na tetesi kuwa Iran imekuwa mstari wa mbele kumsaidia Rais Asad yumkini kwa hisia hizo hizo za Kimadhehebu. Na tetesi nyingine, japo hazikuwa na nguvu sana, zilisema kuwa makundi ya Suni wenye msimamo wa Al-Qaida yalishaingia kwenye uwanja wa mapambano upande wa Wapinzani.

Ni wazi jamii za Waislamu wa Suni na Shia ulimwenguni sasa zitaanza kuhemkwa na kuhamasika na mapambano haya ya kimadhehebu. Ama kwa hakika ni mtihani mkubwa kwa Ulimwengu wa Waislamu!

 Badala ya kugawanyika kwa misingi ya kimadhehebu, Ulimwengu huu wa Waislamu ungehitaji zaidi mshikamano wa Umma ili kuzikabili changamoto lukuki za ulimwengu wa leo ambao unazidi kuongeza nyenzo za kisayansi dhidi ya sera na malengo ya ulimwengu wa Kiislamu.

 Usekula ndio umetamalaki mamlaka ya ulimwengu ukiyalazimisha Mataifa ya Kiislamu kushiriki katika uchumi haramu, utamaduni haramu na kadhalika. Jamii za Kiislamu ulimwenguni zimekuwa na chaguo gumu la maisha, na kwamba zimelazimika kuishi kwa mseto wa itikadi za Uislamu na Usekula!

 Hii ni kusema kuwa zimekubali kula riba huku zikimsujudia Mwenyezi Mungu, zimekubali kuvaa vivazi vya pato la haramu linalotokana na kodi za miradi ya pombe na makasino ndani ya jamii zao huku zikifunga Ramadhani na kuhiji Maka!

 Huu ni mseto usio rasmi wa itikadi unaoweza kufanana na kandambili za “papa na nguru” ambapo mtu huvaa kwa wakati mmoja kiatu kimoja chekundu na kingine cheusi. Ni mseto wa itikadi unaougawa nusu kwa nusu utii kwa Mwenyezi Mungu na Ibilisi aliyelaaniwa.

Tena kuna hatari kuwa Ibilisi amemega sehemu kubwa zaidi ya utii wa Waislamu. Ni uchaMungu wa ‘dizaini’ yake unaoishia katika Swala na visomo vya Qur’an. Kwa kweli, jamii hizi za Waislamu zilihitaji zaidi nguvu ya Umma ili kujikomboa na hali hii ya hatari.

Nguvu ya Umma iliyotarajiwa kuukomboa ulimwengu wa Waislamu kiitikadi ilishapata pigo la itikadi ya Utaifa ambayo, kimsingi, ilibuniwa na maadui wa Uislamu, na, kwa kiasi kikubwa, ilibuniwa ili kuvunjilia mbali dhana ya Umma inayowaunganisha Waislamu ulimwenguni kote.

Jukumu la Waislamu lililofungana na ‘sifa ya Umma bora” ambalo Mwenyezi Mungu amewapa limekuwa gumu kama si zito kana kwamba Waislamu wamebakiza kidogo tu kusema ‘limewashinda’. Kuna dalili kubwa ya Waislamu ulimwenguni kukata tamaa ukiacha harakati za Mujahidina wachache hapa na pale.

ZINDUKA

  • MKUU wa kitengo cha Habari na Malezi cha Chuo Kikuu cha al Mansoura nchini Misri amesema, kuzusha vita baina ya Waislamu kwa kutumia fitna ya kimadhehebu, yaani sunni na Kishia ndilo lengo kuu la Marekani katika njama zake za kuwarafakanisha Waislamu..Shirika la habari la Rasa limemnukuu Amin Said, akisema hayo mwishoni mwa mkutano uliopewa jina la Nafasi ya Vyombo vya Habari katika Kupambana na Ugaidi, ambao ulifanyika kwa lengo la kutafuta njia za kupambana na njama za Marekani.Annuur Na. 1220 JAMADUL AWWAL 1437, IJUMAA , MACHI 11-17, 2016