×
INSHA YA UCHUMAJI KARAFUU (21 Apr 2016)

Assalaam alaykum.
Tunakaribisha insha zinazoelezea shughuli za uchumaji karafuu.

‘Walituchapa fimbo Ukoloni wanakuja kwa sura ya mikataba’

More
3 months 2 weeks ago #2788 by
‘Walituchapa fimbo Ukoloni wanakuja kwa sura ya mikataba’
Na Zinenge Zikulu
Dunia imegawanyika kijiografia, na kila nchi ina rasilimali za kuwafaa watu wake. Mfumo wa maumbile uliogawanya rasilimali umewekwa kwa namna ya kufanya walimwengu wategemeane.
Kutegemeana huku ndiko kunakoshajiisha dhana za biashara na masoko ya kuuza na kununua. Kila nchi inajengeka kwa rasilimali zake. Hakuna nchi iliyoandikwa mbinguni kuja kuendesha maisha ya watu wake kwa kuombaomba.
Bali nchi inaweza kuhitaji msaada wa kuvuna, kukusanya na kuchakata rasilimali zake ili ziwe chanzo cha mapato yote; pato la mtu-mmoja-mmoja, Kaya na Taifa.
Katika kipindi cha ukoloni, Tanzania ilikuwa na nguvu kubwa ya uchumi wa kilimo mikononi mwa wageni. Pamba, Mkonge, Kahawa, Korosho ni mazao yaliyovuma kwa biashara katika soko la kimataifa.
Mabaki ya mashamba ya Mkonge katika Mikoa mbalimbali ni alama ya uchumi huo wa kilimo katika soko la nje. Kwa msingi huo, hata baada ya uhuru, nchi ilijitahidi kuendeleza Uchumi wa kilimo.
Serikali ya Awamu ya Kwanza iliamini kwa kaulimbiu mbalimbali ikiwemo ya Kilimo Uti wa mgongo wa Taifa kwamba Kilimo ndicho kingeweza kuwapatia wananchi hali bora ya maisha na maendeleo.
Hii ni kusema kuwa kwa kutegemea kilimo cha mkonge, korosho, kahawa na pamba na mazao mengine, Tanzania ingeliweza kujitegemea yenyewe kama Taifa.
Hadi mwishoni mwa miaka ya 1970, tuliamini kuwa kilimo kingetimiza malengo yetu ya kiuchumi kwa namna zote; usalama wa chakula, na biashara katika soko la kimataifa, na hata kuvipatia viwanda vyetu malighafi.
Lakini matarajio yetu hayakutimia baada ya kuporomoka kwa sekta ya kilimo. Kufikia mwanzoni mwa miaka ya 1980, usalama wa chakula haukuwepo kabisa, biashara ya nje ikashuka mno, sekta ya viwanda ikaanguka. Kwa lugha ya jumla, tulifilisika kama Taifa.
Badala ya kuzungumza lugha ya maendeleo ya kiuchumi, tukaanza kuzungumza lugha ya kujikomboa kiuchumi. Mikakati ikawa si ya kuendeleza bali ni ya kufufua uchumi kwa maana uchumi ulikufa.
Kumbe baada ya kutupatia uhuru wa bendera, Wakoloni wakashika mpini wa uchumi. Wamebadili staili ya ukoloni kutoka ule wa kisiasa kuja wa kiuchumi.
Walipokuwa watawala wa Tanganyika, mashamba yalikuwa mali yao. Ni wao walioziuzia nchi zao mazao husika ya biashara kwa nguvu kazi yetu ya kuchapwa viboko.
Januari Yusuph Makamba, Waziri wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, alitoa salamu nzito za kuunga mkono jitihada za Rais dhidi ya ufisadi wa rasilimali za nchi wakati Rais alipokuwa ziarani Mkoani Tanga.
Alisema walewale waliotuchapa bakora na kuchukua rasilimali zetu kwa nguvu kabla ya Uhuru ndio hao ambao leo wanakuja kwa sura za Mikataba.
Na wameweka mahakama za Kimataifa za mashauri ya biashara kwa maslahi yao. Tunavaa suti na tai na kumwaga wino sisi wenyewe kwenye makabrasha ya mikataba ambayo hatimaye inatuletea hasara kama nchi!
Makamba alitaka kulitanabahisha Taifa kuwa vita vinavyoendelea dhidi ya ufisadi ni vigumu na kwamba tumsaidie Rais. Kwa upande wake, Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, yeye alikumbushia namna tulivyokosa hata dawa ya meno dukani.
Ni kwa sababu ya uthubutu wa Mwalimu Nyerere wa kuwavimbia au kuwabambia mabepari. Mwalimu aligoma kugeuka jiwe, vita na mabepari vikawa vikali, na mwisho akaona bora ang’atuke madarakani kuliko kusalimu amri kwa mabepari!
Huo ndio wakati ambao Ndugai, bila shaka akiwa mwanafunzi, alihangaika Dodoma yote kutafuta colgate bila mafanikio. Lugha madukani ilikuwa moja-“hamna”. Colgate ilikuwa inatoka kwa mabepari waliozuia vitu vyao kuingia katika nchi ya Julius Nyerere mpaka awasujudie!
Zama hizo zimepita lakini hujuma za wanyonyaji dhidi yetu ziko palepale labda zimebadilika sura tu. Makampuni ya Kimataifa, kwa njia ya mikataba ya uwekezaji, yanaingia na kuchukua rasilimali nyingi huku wananchi hata wale wanaozunguukwa na rasilimali hizo wakizidi kuwa masikini!
Taifa, chini ya Rais Magufuli, limeamua kupambana na wizi au uporaji wa rasilimali za nchi. Hivi ni Vita ambavyo Makamba mtoto alisema, vinafuatiliwa na Mataifa yote.
Walimwengu wanawaangalia Watanzania na hatima ya vita dhidi ya mafisadi wa kimataifa wanasomba rasilimali za nchi yetu. Joseph Butiku alishalitonya Taifa kuwa hawa ndio mabwana wakubwa wanaoshika Uchumi wa Dunia.
Sio makampuni binafsi tu bali nyumba yao zipo serikali za nchi kubwa zinazonufaika na uporaji wa rasilimali zetu! Mataifa makubwa hayana uchumi wa halali na wa haki. Ni uchumi wa kupora rasilimali za wanyonge na kisha kuwapoza kwa ile inayoitwa misaada ya hisani!
Ni wazi tuna changamoto ya kupambana na wale ambao tumezoea kuwaita ‘wafadhili’ au ‘wahisani’ wetu. Rais wetu anaamini kama anavyoamini kila mzalendo kuwa tunachookoa ni kingi au kikubwa kuliko tunachopewa kwa hisani.
Huu ni ujasiri wa aina yake, na ni salamu kwa mabeberu kwamba nchi yetu haiwezi kuishi kwa kuombaomba misaada daima dumu. Sasa imedhamiria kujikomboa kiuchumi.
Twafahamu fika kuwa nguvu za uchumi wa leo wa soko zimeshikwa na hao hao tunaopambana nao. Wapo wanaotupigia mfano wa ugumu wa kupambana na mamba mtoni.
Watatumia hila mbalimbali kutukomoa lakini tujishike na tujiamini. Umefika wakati tuseme kuachiwa mashimo matupu katika ardhi iliyosheheni madini huku umasikini ukizidi kutusakama sasa basi!
Kamati zilizotumwa kuchunguza kadhia za uchimbaji wa madini zimetuzindua kuwa wageni wetu wanaokuja kwa jina la uwekezaji ni wezi. Wanatuibia mchana kweupe.
Japo sisi wenyewe hatuna uwezo wa kuvuna madini yetukwa kiwango cha kututajirisha lakini angalau basi tusiibiwe. Tugawane na wenye uwezo wa kuyachimba alau hamsini kwa hamsini kama alivyosema Mwenyekiti wa Kamati ya Almasi, Hassan Zungu.
Mwafrika amekuwa matatani kwa rasilimali zake mwenyewe. Angola, Congo ameumia na kufa kwa vita vya kunufaisha waporaji wa madini. Tanzania, kwa sababu ya amani na utulivu wake, inaibiwa kwa kalamu zaidi.
Baada ya mikataba ya uchimbaji kusainiwa, milango ya wizi hufunguka. Hadi tunakuja kushituka na kuunda tume za kuchunguza, mizigo mingi ilikwishapita Bandarini na uwanja wa ndege, na hata kwa njia nyingine za magendo.
Sasa tumeshituka na wao wametaharuki kana kwamba hawaamini kama tungeweza kujua walichokuwa wakikifanya. Tumekamata madini yetu. Rais ameshauri yanaweza kuhifadhiwa benki kuu.
Haya ni maoni ya kiongozi wetu. Wachumi nao wanaweza kutusaidia kimawazo na kitaalamu kuhifadhi utajiri wetu huku tukinufaika nao. Tusiulalie utajiri wa madini kama nyoka. Wachumi waumize vichwa tupate masoko yenye faida.
Tutawalaumu wasomi wetu kama madini yatabaki bila masoko huku tukilia njaa! Mabalozi wetu nje ya nchi wafanye kazi ya ziada kuyanadi madini yetu. Wawe madalali hasa wa kuunadi utajiri wa madini ili kupata wateja wanaoweza kununua na kuja kuwekeza katika sekta ya madini kwa misingi ya haki na uadilifu. Hicho ndicho kibarua cha diplomasia ya Uchumi walichopewa.
Kwa vyovyote, hila zitafanyika ili tukose masoko lakini katika dunia hii ya utandawazi, masoko ni mengi. Tusianze kukata tamaa kwamba madini yetu yasipochukuliwa na wanaotuibia hakuna pengine pa kuyauzia!
Maoni tuma 0753736831

Please Log in or Create an account to join the conversation.

Moderators:
Time to create page: 0.495 seconds