×
INSHA YA UCHUMAJI KARAFUU (21 Apr 2016)

Assalaam alaykum.
Tunakaribisha insha zinazoelezea shughuli za uchumaji karafuu.

Al-Khidhri alikuwa nani? Nabii, Walii au Malaika?

More
3 years 5 months ago - 3 years 5 months ago #2035 by Al-Jabri
Maswahaba wasema alihudhuria Mazishi ya Mtume (saw)
Ana umbile la ujana na Utuuzima, ana ndevu nyeupe tupu, Ana Uhai mrefu!
Sheikh Abdul Qadir Jaylani naye asema alikutana naye


Na Maulamaa, Mfasiri S. Hussein

Al-Khidhri ni kiumbe wa kutatanisha aliyetajwa katika Sura ya 18 ya Qur’an (Surat al-Kahf), aya ya 62 hadi ya 82. Ni kiumbe aliyefanya mambo ya ajabu nje ya Elimu aliyokuwa nayo Nabii Musa aliyepata fursa ya kuongozana naye.
Katika Kitabu chake, The History of al-Tabari, Mwanazuoni na Mwanahistoria wa Kipersia na mfasiri wa Qur’an, Muhammad ibn Jarir al-Tabari ameandika kuhusu Al-Khidhri katika sura iitwayo, “Kisa cha Al-Khidhri na Historia yake, na Historia ya Musa na Mtumishi wake, Joshua.”
Katika maudhui ya Kitabu hicho, Al-Tabari anatoa maelezo ya hadithi ya kale inayomuhusu Al-Khidhri. Mwanzoni mwa Sura hiyo, al-Tabari anafafanua kuwa Al-Khidhri aliaminika kuwa ni mtoto wa mtu mmoja aliyemwamini Ibrahim au mfuasi wa Ibrahim ambaye aliondoka pamoja na Ibrahim pale alipohama Babylon.
Aidha Al-Khidhri anaaminika kuwa alikuwa na mamlaka katika himaya ya Mfalme Dhul-Qarnaiyn ambaye katika Kitabu hiki anatambuliwa kama Mfalme Afridun.
Hivyo, al-Khidhri ni mtu aliyeishi kabla ya enzi za Nabii Musa. Katika kitabu hicho, Al-Khidhri anatajwa kukutana na Mto wa Maji ya Uzima au maji ya uhai.
Akiwa hajui vilivyomo ndani ya mto huo, akanywa maji yake, na, hivyo, kuwa mtu mwenye uhai mrefu. Ina maana kuwa uhai wake mrefu umetokana na maji ya uhai aliyokunywa bila yeye mwenyewe kujua.

Kuba ya Al-Khidhri, Hekalu la Mji mkongwe wa Jerusalem
Pia Al-Khidhri amekuwa akifananishwa na Elijah, lakini Al-Tabari anamtofautisha na Elijah kwa kusema kuwa al-Khidhri ni Mpesia na Elijah ni Muisraili.
Al-Tabari anaelekea zaidi kuamini kuwa Al-Khidhri aliishi katika kipindi cha Afridun (Dhul-Qarnain) kabla ya Musa kuliko kuamini kuwa aliandamana na Ibrahim, na kuliko kuamini kwamba alikunywa maji ya Uzima (Water of Life).
Al-Tabari haelezi wazi kwa nini amependelea kuamini hivyo, bali anaonekana kuipendelea isinadi ya kisa cha kwanza (cha enzi za Afridun-Dhul-Qarnain) kuliko kisa cha pili.
Maelezo mbalimbali ya Kitabu cha al-Tabari ama yanalingana zaidi au kidogo na maelezo ya Qur’an. Hata hivyo, katika hadithi za Al-Tabari, inaelezwa kuwa Musa alidai kuwa na elimu kubwa zaidi ya mtu yoyote duniani.
Mwenyezi Mungu akamsahihisha kwa kumwambia kuwa amtafute al-Khidhri ili kuipima elimu yake. Musa akaambiwa aende na samani aliyeokwa, na mara atakapoona samaki huyo katoweka, basi hapo ndipo atakapomuona al-Khidhri.
Musa akatoka na mtu wa kuandamana naye, na walipofika sehemu fulani, samaki huyo aliyeokwa akapata uhai na kutorokea majini. Ni mahali hapa ambapo Musa na mtu aliyeandamana naye wakakutana na al-Khidhri.
Katika Qur’an, kiumbe huyu ametajwa kama mja mchaMungu aliyekuwa na ilimu nyingi kutoka moja kwa moja kwa Mwenyezi Mungu. “Basi wakamkuta mja katika waja wetu Tuliyempa Rehema kutoka Kwetu, na tuliyemuelimisha ilimu (nyingi) zinazotoka Kwetu.” (18:65)

Katika simulizi mbalimbali za Waislamu na wasiokuwa Waislamu, Khidhri ameelezewa kama Nabii au Walii au hata Malaika. Nchini India, Alkhidhri amefananishwa na Vishnu.

Nchini Iran, amefananishwa na Sorush, Nchini Amenia, amefananishwa na Mtakatifu Sarkis, “the Warrior” na amefananishwa na Yohana Mbatizaji. Na kule Asia Minor, amefananishwa na Mtakatifu George, na kadhalika.

Katika sherehe yake ya tafsiri ya Qur’an, Tafhimul-Qur’an, The Meaning of the Qur’an, Mfasiri Sayyid Abul ‘Ala Maududi yeye kasema kuwa yumkini Al-Khidhri alikuwa ni Malaika kwa sababu ya mambo ya ghaibu aliyoyafanya.

Anasema, katika Sheria na kanuni za kibinadamu huwezi kumuhukumu mtu kabla hajatenda dhambi kama alivyofanya Al-Khidhri kwa yule kijana aliyemuua kwa sababu atakuja kuwaaharibu wazazi wake. Tangu hapo, mwanadamu wa kawaida asingeweza kujua maisha ya baadae ya mtoto huyo. Huu ni mtazamo wa Maududi.

Kilugha, kwa sababu ya kufanana kilugha kati ya jina al-Khidhri na jina al-akhdar la Kiarabu lenye maana ya kijani, maana ya jina Al-Khidhri, mara nyingi, hasa katika lugha ya mazungumzo, na hata kitaaluma, huwa ni “Mtu wa Kijani”.

Baadhi ya Maulamaa wanaikataa maana hiyo. Hata hivyo, Maulamaa wengine wanaonesha uwezekano wa kumfananisha na mtu mmoja wa Mesopotamia, Utnapishtum. Kwa mujibu wa mtazamo mpya, Khidhri si neno la Kiarabu.

Katika Jamii ya Waislamu wa Suni, ingawaje Wanazuoni wa Sunni wanakhitilafiana rai juu ya iwapo al-Khidhri bado yuhai, lakini miongoni mwa Masufi wa Kisunni, kuna maafikiano kuwa al-Khidhri bado yuhai huku watu wa kuheshimika, na Masheikh, na Maimamu wakubwa wakidai kuwa wamekutana ana kwa ana na mja huyu, Al-Khidhri.
Mifano ya watu waliosema wamekutana na al-Khidhri ni Sheikh Abdul Qadir Jaylani, Sheikh al-Nawawi, Ibn Arabi, Sidi Abdul Aziz ad-Dabbagh na Ahmad ibn Idris al-Fasi.
Kwa mujibu wa Lata’if al-Minan (1:84-98), kuna maafikiano miongoni mwa Masufi kuwa al-Khidhri bado yuko hai.
Katika duru za Twariqa, watu wa Twariqa, Zawiyyah, Idrisiyya, Muridi, wanampa al-Khidhri nafasi adhimu katika maono yao ya ndani na mawanda yao ya kiroho. Katika jamii ya Masufi, al-Khidhri ni mtu yoyote anayepata nuru inayotoka moja kwa moja kwa Mwenyezi Mungu bila taamuli ya kibinadamu.
Kwa mujibu wa Sufi mmoja wa Sri Lanka, Bawa Muhaiyaddiin, Al-Khidhri alikuwa ni mja aliyefanya jitihada za muda mrefu za kumtafuta Mungu hadi Mwenyezi Mungu, kwa rehema Zake, akamtuma Jibril kwenda kumuongoza.
Jibril akajitokeza kwa Al-Khidhri kama mwalimu wa kibinadamu mwenye hekima, na al-Khidhri akampokea Jibril kama mwalimu wake. Jibril akamfundisha al-Khidhri vilevile kama al-Khidhri alivyokuja kumfundisha Musa baadae kwa kufanya matendo ambayo yalionekana kama ni ya kidhalimu.
Al-Khidhri akavunja mara kwa mara ahadi ya kutosema jambo la kupinga matendo ya Jibril, na bado hakuwa amejua kwamba mwalimu yule wa kibinadamu alikuwa ni Jibril.

Kisha Jibril akafafanua matendo aliyoyafanya, na akabainisha umalaika wake kwa al-Khidhri. Ndipo Al-Khidhri alipotambua kuwa kumbe Mwalimu yule alikuwa ni Malaika Jibril aliyemjia kwa sura ya kibinadamu.

Picha ya Al-Khidhri iliyochorwa Karne ya 17 Katika Sura ya 18, aya ya 65-82, Musa anakutana na mja miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu ambaye Mwenyezi Mungu anasema, “Tuliyempa Rehema kutoka Kwetu, na tuliyemuilimisha ilimu (nyingi) zinazotoka Kwetu.”

Maulamaa wa Kiislamu wanamtambua kama al-Khidhri ingawaje hatajwi waziwazi katika Qur’an, na hakuna utajo wa wasifu wake wa kimaumbile. Qur’an inaeleza kuwa Musa na Al-Khidhri walikutana kwenye makutano ya bahari.

Kukutana kwao kulitanguliwa na tukio la ajabu la samaki wa chakula cha safari cha Musa na Kijana wake kutorokea baharini. “Na walipofika mbele, (Musa) akamwambia kijana wake, “Tupe chakula chetu cha asubuhi; maana tumepata uchovu katika safari yetu hii.

(Kijana wake) akasema, “unaona basi! Pale tulipopumzika katika mlima, nimesahau kukupa habari ya yule samaki. Na hakuna aliyenisahaulisha isipokuwa Shetani, nisikumbuke. Naye (samaki) akashika njia yake baharini kwa namna ya ajabu.

(Musa) akasema: ‘Hapo ndipo tulipokuwa tunapataka.’ Basi wakarudi nyuma kwa kufuata njia yao (ileile). Basi wakamkuta mja katika waja Wetu….”

Baada ya kukutana, Musa akaomba ruhusa ya kuongozana na Mja huyu wa Mwenyezi Mungu ili aweze kujifunza kwake ‘ilimu sahihi ya yale ambayo amefundishwa.

Mja huyo akamwambia Musa kwa uzito kuwa asingeliweza kuvumilia kuandamana naye kwani asingeliweza kuyavumilia mambo asiyoyajua undani wake.

Musa akaahidi kuwa angekuwa mvumilivu inshaAllah. Mja huyo akatahadharisha kuwa kama wangeongozana basi asingependa Musa amuulize-ulize kuhusu yale ambayo angeyaona.

Wakatoka pamoja, na walipopanda jahazi, Al-Khidhri akatoboa jahazi hilo. Musa akakiuka ahadi yake kwa kushindwa kulivumilia jambo hilo. Akauliza, mbona tena unatoboa jahazi, unataka kuzamisha watu ? Hakika umefanya jambo baya.

Mja huyo akamkumbusha Musa kuhusu ile tahadhari aliyompa. Sikukwambia kwamba huwezi kuvumilia kuongozana nami? Musa akaomba samahani kwa kusahau.

Baada ya tukio hilo, Mja huyo akafanya tukio jingine la kumuua kijana mmoja. Kwa mshangao na masikitiko, Musa akalalamika. Al-Khidhri akakumbushia tena ile tahadhari yake. Musa akaahidi kuwa hatovunja tena ahadi yake.

Wakaendelea na safari yao hadi wakafika katika mji ambao wenyeji wake walishindwa kuwakirimu. Licha ya hivyo, Mja huyo akainua ukuta uliobomoka katika mji huo.

Kwa mara nyingine, Musa akamuona Khidhri kama mtu wa ajabu, na akavunja ahadi ya uvumilivu kwa mara ya tatu, akihoji, kwa nini asiwatoze watu wa mji huo malipo ya kazi hiyo?

Mja huyo akamwambia Musa, hapa ndipo tunapofarakiana mimi na wewe. Ngoja sasa nikufahamishe undani wa mambo ambayo wewe hukuweza kuyavumilia.

Kuhusu Jahazi, akamwambia liliharibiwa ili kuwakinga wamiliki wake wasiangukie mikononi mwa mfalme ambaye alikuwa akikamata kila jahazi kwa nguvu. Tukio hili ni ishara kuwa kumbe jambo linaloweza kuonekana baya na la shari huweza kuwa na kheri na matokeo mazuri kabisa.

Na kuhusu kijana, wazazi wake walikuwa waumini, na ilihofiwa kuwa asije akasababisha wazazi wake waasi na kukufuru.Mwenyezi Mungu angewajaalia mtoto mwingine mwema ambaye angepambika kwa utakaso, mapenzi na utii.

Na kuhusu Ukuta ulioinuliwa, chini ya ukuta huo kulikuwa na hazina ya mayatima ambao baba yao alikuwa mcha Mungu. Akiwa kama mjumbe aliyetumwa na Mwenyezi Mungu, Al-Khidhri akauinua ukuta huo, hapa Mwenyezi Mungu akiulipa wema wa baba mchaMungu wa mayatima hao ili mayatima hao wakikua waione na kuitumia hazina yao.


Al-Khidhri alivyoelezewa katika Hadiyth

Miongoni mwa dalili kuhusu maisha ya al-Khidhri ni riwaya mbili; moja iliyosimuliwa na Imam Ahmad ibn Hanbal, katika Al-Zuhd ambapo Mtume ameripotiwa kusema kuwa Elijah na al-Khidhri hukutana kila mwaka katika Mwezi wa Ramadhani mjini Jerusalem.

Na riwaya nyingine ilisimuliwa na Ya’qub ibn Sufyan kutoka kwa Umar kwamba mtu aliyeonekana kuongozana naye alikuwa ni al-Khidhri. Ibn Hajar akabainisha kisa cha kwanza na cha pili kuwa vyote ni sahihi. Taz. Fath al-Bari (1959 ed. 6:435).

Akaendelea kutaja riwaya nyingine sahihi iliyosimuliwa na Ibn Asakir kutoka kwa Abu Zur’a al-Razi ambapo Abu Zur’a al-Razi alikutana na al-Khidhri mara mbili; ya kwanza wakati wa ujana wake, na ya pili wakati wa uzee wake, lakini al-Khidhri mwenyewe alikuwa hakubadilika haiba.

Al-Khidhri anaaminika kuwa na haiba ya kijana na mtu mzima, mwenye ndevu ndefu nyeupe. Kwa mujibu wa waandishi kama Abdul Haq Vidhyarthi, al-Khidhri ndiye Xerxes (asichanganywe na Xerxes I) ambaye alitoweka baada ya kuingia katika mikoa ya kanda ya Ziwa ya Sistan.

Mikoa hiyo inajumuisha nchi za majimaji za mpakani mwa Iran na Afghanistan hivi leo, na baada ya kupata eneo la kuishi, akaazimia kuishi maisha yake yote yaliyosalia akimtumikia Mungu na kuwasaidia wale waliopita katika njia ya kumfuata Mungu.
Muhammad al-Bukhari kasimulia kuwa al-Khidhri alipata jina hili baada ya kujitokeza juu ya uso wa ardhi ambao uligeuka rangi ya kijani baada ya yeye kujitokeza hapo.
Kuna riwaya kutoka kwa Bayhaqi kwamba al-Khidhri alihudhuria mazishi ya Mtume Muhammad, swallallahu alayhi wa sallam, na alitambuliwa na Swahaba Ali miongoni mwa Maswahaba waliokuwepo.
Al-Khidhri alikuja kuonesha huzuni na majonzi yake juu ya kifo cha Mtume Muhammad. Tukio la al-Khidhri kuhudhuria mazishi ya Mtume Muhammad, swallallahu alayhi wa sallam, linaelezwa hivi:
Mtu aliyeonekana kuwa na nguvu, haiba nzuri na mtanashati mwenye ndevu ndefu nyeupe alijitokeza akiwaruka mgongoni watu (waliokaa) hadi akafika pale ulipolazwa mwili wa Mtume Muhammad. Huku akilia kwa uchungu, aliwageukia Maswahaba na kuomboleza. Ali ibn Abi Talib akasema, mtu huyo alikuwa ni al-Khidhri.
Katika simulizi nyingine, al-Khidhri alikutana na swahaba mmoja katika eneo la Ka’aba na akamfundisha swahaba huyo dua ambayo ni yenye thawabu sana pale inaposomwa baada ya Swala za Faradhi. Hii imesimuliwa na Imam Muslim.

Ukinyoa upara usiokote madoriani
Attachments:
Last edit: 3 years 5 months ago by Al-Jabri.

Please Log in or Create an account to join the conversation.

More
2 years 1 month ago #2420 by king hasheem
Naomba nieleweshwe

Please Log in or Create an account to join the conversation.

More
2 years 1 month ago #2421 by Al-Jabri

king hasheem wrote: Naomba nieleweshwe

Soma kikamilifu hiyo makala utafahamu insha-Allah.

Ukinyoa upara usiokote madoriani

Please Log in or Create an account to join the conversation.

More
2 years 1 month ago #2422 by king hasheem
Tafadhali naomba majibu Elijah ni nani ?

Please Log in or Create an account to join the conversation.

Time to create page: 0.443 seconds