×
INSHA YA UCHUMAJI KARAFUU (21 Apr 2016)

Assalaam alaykum.
Tunakaribisha insha zinazoelezea shughuli za uchumaji karafuu.

Athari na nafasi ya ushirika mwema katika tabia ya uzalendo

More
11 months 22 hours ago #2709 by
Na Sheikh Muhsin Elsayid Mohamed - Al Azhari Sharif,
Shukurani zote anastahiki Mwenyezi Mungu (S.W) Mola wa viubwa vyote na mfalme wa pekee siku ya Malipo.

Rehma na Amani zimfikie Mtume na Nabii wa mwisho,Bwana wa wafanya ibada, Ustadhi wa wenye kushukuru, na kiongozi wa watu wema Muhammad (S.A.W), yeye na Jamaa zake, sahaba zake na wote wanaomfuata kwa wema hadi siku ya mwisho.

Ndugu zangu, kwa yakini kuipenda nchi yako ni ukamilifu wa imani, na kuihudumia ni jambo zuri kwa kila mtu mwenye akili timamu.

Hisia za mapenzi ya kweli kwa nchi mar azote hutoka katika moyo wa mtu mzalendo anayejua thamani ya ardhi aliyoamua kuishi iwe kwa kuzaliwa au kwa kuhamia.

Nchi hukusanya mambo mengi zaidi ya ardhi, watu, mazingira, jiografia, na aina ya uongozi, pia hukusanya lugha tunayojivunia na tunayoizungumza, na muongozo wa Mfumo wa maisha tunaoufuata (siasa na dini) tunaufuata, nidhamu tunayoiheshimu na kuaminiana sisi kwa sisi, fikra tunayoijenga kwa ajili yake, malengo tunayoyahakikisha katika nafsi zetu na mwilini mwetu, na elimu tunayoisambaza na kuihimiza.

Mambo hayo yote yamebebwa katika kapu moja la uzalendo, nalo ni jambo zuri na nimtaji mkubwa katika nyoyo zetu kwa ajili ya zama zijazo.

Kwa hivyo basi ni wajibu wa kila mmoja wetukushiriki shughuli anuai za maendeleo ya nchi yake ili kulinyanyua taifa lake, kwani hilo ndilo jahazi linalotubeba sisi sote.

Bwana Mtume (S.A.W) pale alipotoka Makka kwenda Madina, aliitazama Makka akisema; “Namuapia Mwenyezi Mungu (S.W) ewe Makka,kwa hakika wewe ni mji ninaoupenda sana katika miji ya Mwenyezi Mungu (S.W) kwangu, na laiti watu wako wasingenitoa, kwako nisingeondoka” Ameipokea Imamu Tirmidhi, Ibnu Hibban na Twabarani.

Na pale alipohama Mtume (S.A.W) kwenda Madina akarudi kutoka safarini, akazitazama ngazi za Madina, alifanya haraka mnyama wake akasema Ibnu Hajari Al-Askarani katika kutoa dalili za ubora wa Madina na kuipenda nchi na kunasibiana nayo, alikuwa akiomba Dua kwa kusema; “Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu, tupendezeshe sisi Madina kama ulivyotupendezesha sisi Makka au zaidi yake” Hadithi hii imepokelewa na Imamu Bukhari na Muslim.

Na ushirika mwema wenye mafanikio una nafasi kubwa katika kutia nanga kwenye bandari ya maendeleo, na kupata ushindi wa tabia nzuri juu ya uzalendo, ambao hushughulikia maslahi ya nchi.

Hivyo ni wajibu wetu tuamiliane na nchi yetu kwa kuwa sisi ni fungu katika Taifa, kwa kuwa ni mdau na ni sehemu ya nchi.

Kila mwanajamii anatakiwa kuchangia maendeleo ya nchi yake,sanjari nakuzoeana na kupendana kati ya watu wake,kwani hayatimii hayo isipokuwa kwa kushirikiana kwa wema, kwa kuwa umehimiza Uislamu juu ya kushirikiana na kusaidiana katika mambo mema.

Amesema Mwenyezi Mungu (S.W); “…Na saidianeni katika mambo mema na kumcha Mwenyezi Mungu, nawala msisaidiane katika madhambi na uadui….” Rejea sehemu ya Aya ya pili ya Suurat Al-Maadiah.

Ndugu zangu, kuipenda nchi ni daraja ya juu na thamani kubwa na nzuri ya utu, na ni wajibu wetu kupanda mbegu hii na kuiasisi katika nafsi tangu utotoni, kwa ajili ya kuhifadhi yale yote yanayopatikana katika uzalendo, pamoja na kupambana na changamoto zote zinazoweza kuondoa uzalendo huo.

Ni wajibu wetu wote kukataa na kupinga vyanzo vyote vinavyoharibu uzalendo kwa namna zote na aina zote, na tutakapofanikiwa juu ya hilo tutaweza kuasisi kwa pamoja muonekano wa mafanikio na maendeleo ya jumla kwa jamii yetu kwenye kila sekta inayogusa maisha yetu ya kila siku.

Kwa kuienzi tabia ya kupenda nchi (uzalendo), na kwa kushirikiana kwetu kwenye mambo mema na kukatazana mambo maovu na machafu, basi ndoto yetu ya mafanikiohufikia kilele cha uhalisia wake.

Tusisitize tu kuwa, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuweka nyuma ya migongo yake, yale yote yaliyo kinyume na kuipenda nchi yake.

Jambo lingine muhimu ni kukwepa kila chanzo cha ubaguzi au tofauti za aina zote, ili wasipewe njia maadui kutufarakanisha.

Na pia linguine la kusisitizwa ni lile la kufanya kazi kwa bidii kwa kila mmoja katika nafasi na taaluma yake, kwani kila raia katika nchi yake ni askari miongoni mwa askari wa kupambana na adui ujinga, maradhi na umasikini chini ya mtaji wa rasilimali watu wenye tabia njema, wanaofuata siasa safi, na kuwa na uongozi bora; kwani hayo ndoyo matendo mazuri, na matendo mazuri ni miongoni mwa sifa za mtu mwenye imani.

Basi inatakikana vilevile kwa wote tufanye mambo mema kwa maslahi ya nchi ambayo tunaishi ndani yake iwe Kisiasa, Kiuchumi, Kidiplomasia, Ulinganiaji n.k. ili kunyanyua na kusukuma mbele gurudumu la maendeleoya nchi.

Amesema Mtume (S.A.W);“Hakika Mwenyezi Mungu (S.W) anampenda mmoja wenu anapofanya jambo, basi alifanye kwa ufanisi” Ameitoa Imamu Twabarani na Abuu Yaala.

Jambo linguine ambalo tungependa lisisahaulike kwenye muktadha huu, ni lile la kuyatanguliza maslahi ya juu ya nchi kuliko maslahi ya mtu mmoja, ili tuweze kuipeleka mbele nchi kimaendeleo na kuiepusha na fujo, na kupatikana yale yote mazuri yanayowezekana kwa raia.

Mwisho japo si tamati, tunawausia pamoja na kuziusia nafsi zetu, juu ya umuhimu wa kusimamia nafasi za taasisi kuu za maendeleo ya jamii kwa uwadili na ufanisi, ili kutia moyo roho za kunasibiana na nchi, kupanda roho ya kushirikiana kwenye mambo mema,na hatimaye kuwa na jamii yenye mafanikio ya kila sekta.

Hivyo basi, tunawanasihi juu ya ulazima wa kushikamana na ushirika mwema, ili uweze kusimamia nafasi yake kubwa katika kuienzi tabia nzuri ya kupenda nchi, na haya hayapatakani isipokuwa kwa kusimama kila mmoja katika nafsi yake katika jamii, na awe mwenye kuleta maendeleo upande wa nchi yake.

Kwa hiyo, linalotakiwa kwa mwananchi ni kufanya kazi kwa bidii, na wala asiwe mvivu, kwani kujinasibisha na nchi sio tu kwa kuwa mapenzi bila ya vitendo, bali iwe kwa kutekeleza na kuunga mkono amali zote njema za kuliendeleza taifa husika, na yote hayo yamehimizwa na Uislamu.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atupe Stara waja wake na kukubalika amali zetu, Aamiin.

Wabillah Tawfiiq,

Kama una maoni, Maswali au ushauri, usisite kuwasiliana na Mudir, Egyptian Islamic Center kwa Email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

Ukinyoa upara usiokote madoriani

Please Log in or Create an account to join the conversation.

Time to create page: 0.392 seconds