×
INSHA YA UCHUMAJI KARAFUU (21 Apr 2016)

Assalaam alaykum.
Tunakaribisha insha zinazoelezea shughuli za uchumaji karafuu.

Hikima ya Mwenyezi Mungu kumuumba Ibilisi

More
3 years 9 months ago - 3 years 7 months ago #1843 by Mwinyi
Na Sheikh Prof. Umar Suleiman Ashqar

Ibilisi ndiye chanzo kikuu cha uovu na khasara. Yeye ndiye kinara wa maangamizi katika maisha haya na katika maisha ya Akhera. Hupandisha bendera yake kila wakati na kila mahali. Huwaita watu katika ukafiri na uasi dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema.

Je, kuna hekima gani basi ya kuumbwa kwake? Ibn Qayyim amelijibu swali hili katika Shifa al-Aliif chini ya kichwa, “Katika kuumbwa kwa Ibilisi na majeshi yake, kuna hikima ambayo hakuna yeyote aijuae kikamilifu isipokuwa Mwenyezi Mungu.”

1. Athari za kupambana na Ibilisi na wafuasi wake ndizo zinazoleta ukamilifu wa ibada

Kutokana na hikima hii ndipo utumishi wa Manabii na waja wa Mwenyezi Mungu unapokamilika na kutimia kwa kule kupambana kwao na adui wa Mwenyezi Mungu na kundi lake na kwa kutofautiana na Ibilisi na wafuasi wake. Hii pia inajumuisha kumkasirikia kwao Ibilisi na wafuasi wake.

(Kipengele kingine ni) kule kujikinga kwao kwa Mwenyezi Mungu dhidi ya Ibilisi na kukimbilia kwao kwa Mwenyezi Mungu ili kujikinga na shari na hila za Ibilisi. Kutokana na yote hayo ndipo unapokuja ustawi katika dunia hii na Akhera ambao usingeweza kuja bila hivyo. Pia hikima hiyo hupelekea kufikiwa kwa daraja za juu kabisa za ibada ambazo zisingeliweza kufikiwa kama si kuwepo kwa Ibilisi.

2. Kwa kuwepo Ibilisi, waja wa Mwenyezi Mungu huingiwa na khofu ya dhambi zao

Kuumbwa kwa Ibilisi kumewafanya malaika na binadamu wawe na khofu ya dhambi zao kwani wameona yaliyompata Ibilisi baada ya uasi wake mkubwa. Kuporomoka kwake kutoka nafasi ya juu ya utawala hadi ile ya mashetani kulikuwa kukubwa na kwa moja kwa moja.

Bila shaka, malaika walioshuhudia tukio hilo walipata somo jipya la kumuabudu Mwenyezi Mungu na wakapata funzo jipya la kumtii na kumnyenyekea Mwenyezi Mungu pamoja na kumwogopa. Walikuwa kama watumwa wa mfalme ambao wamemshuhudia mtumwa mwenzao akidhalilika kwa kiasi kikubwa. Wale walioshuhudia tukio hilo, bila shaka, ndio watakaoogopa na kuchukua tahadhari zaidi mbele ya mfalme.

3. Mwenyezi Mungu Kamfanya Ibilisi awe fundisho kwa wale wanaotafakari

Ibilisi ni fundisho kwa wale wote wanaokhalifu amri za Mwenyezi Mungu na ambao, kwa kibri, wanakataa kumtii Mwenyezi Mungu na huku wakifanya matendo ya kumuasi.

Hii ni sawa na vile ambavyo Adam amekuwa mfano kwa wale wote wanaofanya makosa kwamba watubu na kurudi kwa Mwenyezi Mungu kama alivyofanya yeye. Mababa wote wawali, yule wa majini (Ibilisi) na yule wa binadamu (Adam) walitahiniwa kwa dhambi.

Baba mmoja kawa fundisho kwa wale wote wanaodumu katika njia za kumuasi Mwenyezi Mungu bila kutubu wakati ambapo baba mwingine kawa somo kwa yeyote anayeteleza (kwa kutenda dhambi) na kurudi kwa Mola wake. Vielelezo hivi viwili vikubwa vimejaa hikima na mafunzo.


4. Mwenyezi Mungu amemfanya Ibilisi mtihani na jaribio kwa waja Wake

Ibilisi ni kiumbe mkorofi ambaye Mwenyezi Mungu kamtahini mwanadamu kwaye, hivyo kuwapambanua wale wanaojitakasa na wale ambao ni waovu. Mwenyezi Mungu aliwaumba wanadamu kwa udongo. Baadhi yao ni laini, na wengine ni wakavu. Baadhi yao ni wema na wengine ni wabaya. Kwa hali hiyo, lazima pawepo na kitu cha kuwadhihirisha vile walivyo. Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, amesema,

“Mwenyezi Mungu amemuumba Adam kwa gao alilochota kutoka kote ardhini. Hivyo, wanadamu wananasibiana na ardhi, baadhi yao ni laini, baadhi yao ni wakavu, baadhi yao ni wema na baadhi yao ni wabaya.

Kile kilichokuwemo katika chanzo cha asili (kilichotumika kuumbia) pia kimo katika vile vilivyoumbwa kwacho. Ni sehemu ya hikima ya Mwenyezi Mungu kujaalia tofauti hizi ziwepo na zidhihirike.

Lazima pawepo na sababu ya kufanya tofauti hizi zijitokeze. Kuumbwa kwa Ibilisi ni kichocheo cha kupambanua nani ni nani katika viumbe Vyake. Ibilisi ndiye anayebainisha tofauti kati ya wema na wabaya vilevile kama Mitume na Manabii walivyoupambanua mtihani huo.

“Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwaacheni katika hali mliyonayo mpaka apambanue wabaya katika wema.” (3:179). Mitume walitumwa kwa wanadamu wanaowajibika kwa vitendo vyao. Baadhi ya watu ni wema na wengine ni wabaya. Mitume wakawafungamanisha wema kwa wema na wabaya kwa wabaya.

Ni hikima isiyo na ukomo ya Mwenyezi Mungu inayoyachanganya makundi haya mawili katika dunia hii ya mtihani na majaribio. Kisha, katika ulimwengu wa milele, makundi hayo yatagawanyika, kila kundi liende kwenye makazi yake kwa kuzingatia ile hikima kubwa ya Mwenyezi Mungu na kwa kudra Yake yenye kushinda.

5. Kuumbwa kwa Ibilisi kwadhihirisha uwezo kamili wa Allah kuumba viumbe kwa kuvitofautisha

Kwa kumuumba Ibilisi, Mwenyezi Mungu anadhihirisha kuwa Yeye ana uwezo kamili wa kuumba mfano wa Jibril na malaika wengine na Ibilisi na mashetani wengine. Hii ni moja ya ishara kubwa za uweza Wake na Mamlaka Yake. Kaumba viumbe kwa kuvitofautisha kama vile mbingu na ardhi, nuru na giza, pepo na moto, maji na moto, joto na baridi, wema na ubaya na kadhalika.

6. Vya badala yake huonesha mema ya wabadala wao

Sehemu ya hikima hii ni kuonesha wema kamili wa mojawapo ya viumbe viwili vinavyotofautina. Viumbe mbadala huonesha mema ya wabadala wao. Laiti kusingelikuwa na kile ambacho ni kibaya, tusingelitambua kile kilicho kizuri. Laiti kusingelikuwa na umasikini, tusingeliweza kuiona thamani ya utajiri.

7. Mitihani ndiyo kipimo cha ukweli wa shukurani

Kwa hikima ya kumuumba Shetani, ni kwamba Mwenyezi Mungu kapenda kuwa shukurani Kwake ziwe za dhati na zifike. Hapana shaka kuwa waja Wake wanaumia kwa kule kuwepo kwa Ibilisi na askari wake.

Mtihani wa Ibilisi wanaojaribiwa nao hupelekea kuwepo kwa aina ya shukurani ambayo isingekuwepo bila ya kuwepo Ibilisi. Linganisha Adam alitoa shukurani mara ngapi kwa Mwenyezi Mungu wakati akiwa ndani ya pepo kabla hajafukuzwa, na mara ngapi alitoa shukurani baada ya huzuni yake; alitoa shukurani za dhati na akatubu kwa Mwenyezi Mungu na (vyote) vikapokelewa.

8. Katika kuumbwa Ibilisi kuna mambo mengi ya ibada

Ibada hizo ni pamoja na kumpenda Mwenyezi Mungu, kumuamini, kuwa na subira, kupata radhi za Allah na kadhalika. Aina hizi za ibada ndizo zinazopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu.

Aina hizi za ibada hutimizwa kwa njia ya jihadi na kuisalimisha nafsi kwa Mwenyezi Mungu na kuelekeza mapenzi yote kwa Mwenyezi Mungu kabla ya kitu kingine chochote kile. Na jihadi ndio kilele cha ibada na ndiyo inayopendwa mno na Mwenyezi Mungu. Aina hizi za ibada huchukua sura halisi kwa kule kuwepo kwa Ibilisi na kundi lake. Hakuna awezaye kuhesabu faida zote za kipengele hiki isipokuwa Mwenyezi Mungu.

9. Kuumbwa kwa Ibilisi kwadhihirisha ishara za Mwenyezi Mungu pamoja na maajabu ya Uweza Wake

Katika kuwaumba viumbe wanaowapinga, kuwakana na kupambana na Mitume Wake, Mwenyezi Mungu amefungua mlango wa kuiendea njia ambayo kwayo amebainisha ishara Zake nyingi, uweza Wake, maajabu ya ulimwengu aliouumba na vilivyomo.

Ishara hizi kubwa zinafanya kule kuwepo kwa Ibilisi na askari wake kuwa jambo linalopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu kuliko kutokuwepo kwao. Ishara hizi ni pamoja na mafuriko ya zama za Nuhu, kugawanyika kwa bahari, ‘fimbo ya Musa, kumnusuru Ibrahim na moto na ishara nyingine nyingi ambazo zinathibitisha Uweza wake, Ilimu na Hikima Yake mambo ambayo yasingejitokeza kama wasingelikuwepo viumbe wanaompinga Yeye (Mwenyezi Mungu).

10. Ibilisi kuumbwa kwa moto ni ishara

Moto na vitu vya moto vyaweza kutumika kuunguzia, kuwatishia wengine au kufanyia ufisadi. Lakini moto pia hujumuisha mwanga na nuru. Mwenyezi Mungu ndiye anayevitoa vyote hivi viwili katika moto. Vivyo hivyo, kaumba kutokana na udongo wa ardhini wanadamu wema na wabaya, laini na wakavu, wekundu, weusi na weupe. Hii ni dalili ya wazi na ishara ya Uweza Wake na Shani Yake. Na ni ishara zinazoonesha kuwa,

Hakuna chochote mfano Wake, naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)


11. Kuumbwa kwa Ibilisi kwadhihirisha maana ya Majina mengi ya Mwenyezi Mungu

Nyingi miongoni mwa sifa za Mwenyezi Mungu zinadhihiri kwa njia ya kuumbwa Ibilisi, kama vile Mporomoshaji wa daraja (Mwenye kutweza, kushusha cheo), Mpandishaji wa daraja (Mwenye kukweza), Mtukuzaji, Mdhalilishaji, Hakimu, Mtenda haki, Mlipizaji kisasi, na kadhalika. Majina haya hutaja maana zinazoambata nayo ambazo hujitokeza kwa njia ya Hukumu Zake kama vile Sifa Zake za wema, uvumilivu, huruma na kadhalika. Ni jambo la lazima kwamba majina ya aina zote (ya Mwenyezi Mungu) yadhihiri hapa duniani.

12. Kuumbwa kwa Ibilisi kwadhihirisha utawala na mamlaka kamili ya Allah juu ya mambo ya ulimwengu huu

Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utawala na mamlaka kamili juu ya ulimwengu huu. Uweza wake kamili maana yake ni Uweza wa kuutawala ulimwengu vyovyote vile, hiyo ikijumuisha vipengele vya kuadhibu, kulipa, kudhalilisha, kufanya uadilifu, kurehemu, kutukuza na kudunisha. Aina zote za viumbe (wema na wabaya) lazima wawepo ili vipengele vyote hivyo vidhihirike.


13. Kuwepo kwa Ibilisi kwatokana na kutimia kwa hikima ya Mwenyezi Mungu

Mwingi wa Hikima ni mojawapo ya Majina ya Mwenyezi Mungu. Kuwa na hikima ni moja ya Sifa Zake. Hikima hii yahitaji akiweke kila kitu mahala pake sahihi ambapo hakuna kitu kingine chochote kitakachopafaa, na tena kwa uwiano (na vingine). Yeye ndiye aliyeamua kuweka (viumbe) viwiliviwili visivyo na sifa zinazofanana.

Je, Hikima Yake ingetimia bila kufanya hivyo? Kwa hiyo, kuwepo kwa aina zote mbili za viumbe ni matokeo ya Hikima Yake isiyo na Ukomo kwa hali ileile kama ilivyo ishara ya Uweza Wake usio na kikomo.

14. Utukufu ni wa Allah kwa kile ambacho Amekizuia na kukidunisha

Mwenyezi Mungu ndiye anayestahiki kutukuzwa kwa kila jambo miongoni mwa mambo Yake, kwa Uadilifu Wake, kwa Kuzuilia Kwake, Kudunisha Kwake, Kunyanyua Kwake, na kudhalilisha Kwake. Vivyo hivyo, Yeye ndiye anayestahiki kutukuzwa kwa kuruzuku Kwake, kutukuza Kwake, na kukweza Kwake. Utukufu Wake hutimia katika mambo yote hayo. Yeye hujitukuza kwa yote hayo.

Malaika, Mitume na waja nao pia humtukuza Yeye. Yote hayo ndiyo yanayotimiza Utukufu Wake. Katika kuumba Kwake, imetimia Hikima Yake vilevile kama ulivyotimia Utukufu Wake. Haijuzu kuukana utukufu Wake kama ambavyo mtu hawezi kuikana Hikima Yake.

15. Kwa Kumuumba Ibilisi, Mwenyezi Mungu kawaonesha waja Wake upole na subira Yake

Kutokana na hikima ya kuumbwa kwa Ibilisi, Mwenyezi Mungu kapenda kuwaonesha waja Wake upole Wake, subira Yake, huruma Yake, ukarimu Wake na kadhalika.

Ili vyote hivyo vidhihirike, ilihitajika waumbwe viumbe wanaomshirikisha, wanaopinga utawala Wake, wanaofanya juhudi za kupinzana Naye na wanaofanya kazi ya kumghadhibisha. Baadhi hufikia hata kushindana na Mwenyezi Mungu katika Uungu Wake.

Licha ya hivyo, bado Mwenyezi Mungu huwaruzuku watu hao vitu vizuri, afya nzuri, riziki na kadhalika. Na anawaita wafuate njia ya kheri na kuacha uovu na ushirikina.

Hata hivyo, bado Yeye huwaruzuku neema zote hizo, huitikia maombi yao, huwaondoshea madhara, na huenda nao polepole katika kukabiliana na ukafiri, ushirikina na uovu wao. Hebu ona ni kiasi kikubwa kilioje hiki cha Utukufu na Hikima alichonacho Mwenyezi Mungu kwa yote hayo.

Naye huwa kipenzi cha waja Wake huku nao wakitambua ukamilifu wake. Imo (Hadith) katika Sahih (Muslim) kwamba Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, amesema,

“Hakuna mwenye subira kwa uchungu anaousikia kama Mwenyezi Mungu. Wanamzushia eti ana mtoto lakini badoYeye huwapa riziki.”

Pia imo (Hadith) katika Sahih (Bukhari) kwamba Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, kasimulia kutoka kwa Mola wake,

“Mwenyezi Mungu amesema, “Mwanadamu kanitusi, naye hakuwa na haki ya kufanya hivyo. Na kanikadhibisha, naye hakuwa na haki ya kufanya hivyo. Ama kuhusu kunikadhibisha eti anasema, “(Mwenyezi Mungu) hataniumba tena kama Alivyoniumba mwanzo.’ Ambapo huko kuumba mwanzo si kwepesi zaidi kuliko kuumba tena.

Ama kuhusu kunitusi, hii ndiyo kauli yake , ‘Mwenyezi Mungu kajifanyia mtoto,’ ilahali Mimi ni Mpweke, Wa milele, Sikuzaa wala Sikuzaliwa. Na hakuna yeyote anayefanana na Mimi.’”1 Pamoja na kumtusi na kumkadhibisha huko Mwenyezi Mungu, bado Yeye huwapa riziki makafiri katika dunia hii. Huwaponya wanapougua. Huwaita katika njia ya kuingia peponi. Hupokea toba yao pale wanapotubu. Hubadili mabaya yao kuwa mema. Ni Mpole kwao wakati wote. Amewawezesha kuwa na sifa za kupokea ujumbe Wake.

Anawaamrisha wawe laini (waungwana) katika kusema na wawe wapole. Al-Fadhl ibn Lyaadh amesema, “Hakuna usiku ambao giza hutanda bila Mwenyezi Mungu kusema, “Ni nani mkarimu zaidi Yangu? Viumbe huniasi huku Mimi nikiwalinda vitandani mwao kana kwamba hawakuniasi. Na naendelea kuwalinda kana kwamba hawakutenda dhambi. Na nawalea utadhani hawakutenda dhambi. Mimi humkirimu riziki mtenda dhambi. Na namruzuku kwa huruma yule anayetenda dhambi. ‘Je kuna yeyote ambaye huniita nami nisimuelekee? Je yupo aombaye Nami nisimpe? Mimi ndiye Mkarimu na ukarimu unatoka Kwangu.

Nami ndiye Mwenye cheo cha utukufu na cheo hutoka Kwangu, kwamba namruzuku mja chochote anachoniomba. Na nampa kile ambacho hakukiomba. Na katika cheo cha utukufu wangu, Namruzuku kama vile hakuniasi. Kiumbe atakimbilia wapi Nisimpate? Na mlango Wangu upi watakaotokea waovu?’”

Kuna Hadith Qudsi inayosema: “Mimi na wanadamu na majini tupo katika kadhia kubwa: Mimi ndiye niliyewaumba halafu wao wanaabudu wengine badala Yangu. Mimi ndiye ninayewaruzuku halafu wao wanawashukuru wengine.”
Last edit: 3 years 7 months ago by Mwinyi.

Please Log in or Create an account to join the conversation.

Time to create page: 0.409 seconds