×
INSHA YA UCHUMAJI KARAFUU (21 Apr 2016)

Assalaam alaykum.
Tunakaribisha insha zinazoelezea shughuli za uchumaji karafuu.

Ni kwa namna gani Shetani alimgwaya Umar Ibn Khattab?

More
3 months 2 weeks ago #2799 by
Na Shuaybu Hussein,
Katika mapokeo sahihi, Mtume, swallallahu alayhi wa salam, alimwambia Swahaba wake, Umar bin Khattab, “shetani akikuona, anageuza njia.” Haya ni maneno yaliyoashiria mafanikio makubwa kwa Umar kwani kukimbiwa na Shetani, adui yetu mkubwa, ni kushinda vita muhimu zaidi kuliko zote katika dunia hii.

Lakini ni kwa vipi Umar alikimbiwa na shetani ambaye ni adui king’ang’anizi wa mwanadamu aliyekula kiapo cha kuwapoteza wanadamu isipokuwa wachache.

Undani wa ushindi wa Umar dhidi ya Shetani unabebwa na ukweli kuwa kwanza Umar alipambana na nafsi yake na kuhakikisha kuwa haimpi nafasi shetani.

Sahaba mmoja anasema siku moja, wakati yeye akiwa nyuma ya Umar wakiwa wamekingwa na ukuta bila kuonana, alimsikia Umar akijinasihi peke yake, “Ewe Umar, mche Mwenyezi Mungu, tenda haki.”

Kwamba Umar alikuwa anajiambia mwenyewe maneno haya. Kwa maneno mengine, hapa Umar alikuwa anapigana jihadi ya nafsi. Anaikanya nafsi yake isistahabu dhuluma ambayo ndiyo njia ya kumkaribisha shetani.

Kwa msingi huu ndiyo maana Shetani hakujisumbua kumkurubia Umar, na kinyume chake kila alipomuona, aligeuza njia. Hebu sasa tuutazame ushindi huu wa Umar kifalsafa.

Twafahamu, kimaumbile, kwamba Shetani haonekani kwa macho ya binadamu. Qur’an inatufahamisha kuwa yeye na kabila yake wanatuona sisi binadamu lakini sisi hatuwaoni. Ni kwa namna gani Shetani alionekana akikata njia nyingine kumkwepa Umar ikiwa haonekani kimaumbile?

Na, je, ni Umar pekee au wapo watu wengine wengi wanaokimbiwa namna hiyo na Shetani? Ni mambo gani ya kutuonesha kuwa Shetani anamkimbia mtu? Maswali haya matatu ndiyo ya kuidadavulia falsafa ya Shetani kumgwaya Umar.

Tumeshaona kuwa japo Shetani anaishi kimwili lakini binadamu hatumuoni. Kama ni hivyo binadamu anajuaje kuwa Shetani anapomuona yeye hugeuza njia.

Bila shaka ni kwa njia ya matendo ya wanadamu. Kwa mfano, watu wanachelea kufanya jambo ovu kwa sababu yako. Kwamba fulani ana dini sana asijue jambo hili.

Hii ni ishara kwamba Shetani anakuogopa wewe. Zingatia wewe si polisi wa kuwakamata, wala si hakimu wa kuwahukumu, wala huna ilimughaibu ya kuona wanalotaka kulifanya.

Lakini wanakugwaya. Si wao bali ni Shetani aliyewasimamia anayekuogopa wewe. Mfano mwingine, rafiki au jamaa yako yuko baa au kilabuni anakunywa pombe lakini kukuona wewe anajificha usimuone!

Ni kwamba hapa Shetani wa ulevi aliyemsimamia jamaa yako anakuchelea wewe kwa sababu utampa nasaha za kumuongoa rafiki yako. Ndani ya nyumba watu huweza kukugwaya kwamba wana mambo yao yasiyoendana na mwenendo sahihi lakini wanaogopa kuyatenda kwa sababu yako.

Ni kwamba Shetani anayewachochea anakuogopa wewe. Jaalia kahaba yuko mawindoni, anamwita kila mwanaume anayemuona njiani lakini kukuona wewe, ananyamaza, anaogopa hata kukutazama, ni kwamba Shetani aliyemsimamia katika uasherati anakuogopa wewe.

Mifano iko mingi, la muhimu kuzingatia ni kwamba pasiwe na sababu nyingine ya kuogopwa na watu ila imani yako. Wasiogope kwa sababu utawacharaza bakora wala wasiogope kwa sababu utawafukuza kwenye nyumba yako, wala wasiogope kwa sababu utawanyima msaada. Wala wasiogope kwa sababu wewe ni askari.

Wakiogopa hivyo, basi hizo zitakuwa hofu tofauti na ile ya Kiimani. Ishara nyingine ya kukimbiwa na shetani ni kwamba ukiona hubabaiki na maovu, huzidiwi na matamanio mabaya, basi hapo Shetani yuko mbali na wewe, kwamba anaogopa kukusogelea.

Hata unapopita katika njia aliyotega kwa maana ya kukutamanisha mwanamke, au pesa, lakini bado wewe hutetereki kwa vyote hivyo, basi hapo Shetani kakukimbia.

Kuogopwa na shetani ni kilele cha ushindi dhidi ya nafsi, hata hivyo, hiyo haina maana ya kubweteka kwa imani kuwa shetani hawezi tena kukufuata. Bado ataridhika na makosa madogo-madogo ambayo hujilimbikiza na hatimaye kuwa na uzito mkubwa katika mizani.

Ukinyoa upara usiokote madoriani

Please Log in or Create an account to join the conversation.

Time to create page: 0.440 seconds