×
INSHA YA UCHUMAJI KARAFUU (21 Apr 2016)

Assalaam alaykum.
Tunakaribisha insha zinazoelezea shughuli za uchumaji karafuu.

Nini mtazamo wa Uislamu juu ya Utabiri wa Mgombea-Urais ‘atakayekufa Mwaka huu’!

More
3 years 6 months ago - 3 years 6 months ago #1994 by Mfaume
Na Sheikh. Prof. Dkt. Umar Suleiman al-Ashqar

Tunabaini moja ya makosa makubwa ambayo watu wengi huyafanya pale wanapoamini kuwa eti baadhi ya watu kama vile watabiri na waaguzi, huyajua mambo ya ghaibu.

Tunaona watu hao wakienda kwa watabiri na waaguzi hao kutazamia vitu vilivyoibwa au uhalifu uliofanyika. Na wanatazamia mambo ambayo bado hayajawatokea wao na watoto wao.

Wote wawili; yule anayekwenda kutazamia na yule anayefanya kazi ya kutazamia watapata hizaya. Ilimu ya ghaibu iko kwa Mwenyezi Mungu tu. Mwenyezi Mungu hamfichulii ilimu hiyo mtu yeyote isipokuwa yule anayemchagua miongoni mwa waja wake wema:

“Yeye ndiye Mjuzi wa siri; wala hamdhihirishii yoyote siri Yake isipokuwa Mtume Wake Aliyemridhia. Huyo Yeye humuwekea walinzi mbele yake na nyuma yake ili ajue (Mtume) kuwa (Mitume) wamefikisha ujumbe wa Mola wao. Na (Mwenyezi Mungu) anayajua yote waliyonayo na ameidhibiti idadi ya kila kitu.” (72: 26-28).

Kuamini eti mtu fulani ana ilimu ghaibu (au tuseme ana uwezo wa kutazamia mambo yasiyoonekana) ni dhambi na ni imani potofu inayopingana na imani sahihi ya Kiislamu kwamba Mwenyezi Mungu pekee ndiye Mwenye ilimu ya ghaibu.

Kwenda kwa watu fulani-fulani kuulizia fatwa ya jambo linalohusiana na ilimu ya ghaibu ni dhambi kubwa sana. Imenakiliwa katika Sahih Muslim na Musnad Ahmad, kwa mapokeo ya mmoja wa wakeze Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehema na amani zimshukie) amesema,

“Yeyote anayekwenda kwa mtizamiaji (mpiga ramli/bao) na kumuuliza jambo fulani, swala yake haitapokelewa kwa siku arobaini.”

Kuamini yale anayoyasema ni kufuru. Abu Huraira kasimulia, kama ilivyonakiliwa katika Musnad Ahmad, kwamba Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, amesema,

“Yeyote anayekwenda kwa mtizamiaji au mtabiri na kusadiki yale ayasemayo, basi huyo kakadhibisha yale yaliyoteremshwa kwa Muhammad.”


Katika Sharh al-Aqiida at-Tahaawiya, inaelezwa, “wanajimu huangukia katika kundi hili la watazamiaji kwa mujibu wa baadhi ya wanazuoni wakati ambapo wengine husema tu kwamba maana yake ndiyo inayowahusu wao pia. Na kama hivyo ndivyo inavyokuwa kwa mtu anayemuuliza (mtizamiaji), (hebu fikiria) hali itakuwaje basi kwa huyo mtizamiaji mwenyewe (mpia ramli) anayeulizwa?”

Hii ikiwa na maana kuwa ikiwa yule anayemuuliza mpiga ramli au mtabiri, Swala yake haitapokelewa kwa siku arobaini, na yule ambaye anasadiki anayoyasema mwaguzi/mpiga ramli/mtabiri/, huwa kafiri, hebu fikiria hukumu itakuwaje kwa huyo mwaguzi au mtabiri au mpiga ramli mwenyewe?

Kumuuliza mwaguzi kwa lengo la kumpima? :)

Ibn Taimiya katoa rai kuwa kumuuliza mwaguzi ili kumpima, kuifichua tabia yake halisi na kuyachuja maneno yake ya uwongo na kweli ni jambo linaloruhusiwa.

Dalili yake ipo katika Hadith iliyomo katika vitabu viwili vya Sahih: Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, alimuuliza ibn Sayaad. Mtume wa Mwenyezi Mungu alimuuliza bwana huyo, “nini kinachokujia?” Akajibu, “Wakati mwingine, mtu mkweli na wakati mwingine, mtu mwongo hunijia.” Kisha akamuuliza, “Unaona kitu gani?” Akajibu, “naona kiti cha enzi juu ya maji.” Mtume, swallallahu alayhi wa sallam , akasema, “Nimeficha kitu fulani kutoka kwako.” Akasema, “hiyo ni al-Dukh.” Mtume (saw) akasema, “nakuombea udhalilike. Kamwe hutapanda daraja. Wewe si chochote bali ni ndugu moja na watabiri.” Unaweza kuona hapa kuwa Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, aliuliza maswali hayo ili kuwabainishia watu hali halisi ya bwana huyo.

Wanajimu

Hawa ni watu wanaotumia nyota au sayari kutabiri mambo ya dunia. Hili ni jambo lililoharamishwa na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna. Kwa kweli mitume wote wa Mwenyezi Mungu wameharamisha jambo hilo. “Wala mchawi hafaulu popote afikapo.” (20:69). Mwenyezi Mungu pia anasema,

“Huwaoni wale waliopewa sehemu ya Kitabu? Wanaamini masanamu (jibt) na miungu bandia (twaghuut).” (4:51). Umar ibn al-Khattab alisema kuwa jibt ni uchawi

Dhana Potofu

Baadhi ya watu hudai kuwa eti wakati mwingine wanajimu, watabiri, wapiga bao na wengineo, huwa ni wakweli. Kuwa kwao wakweli katika mambo mengi ni aina ya udanganyifu wa mwanadamu.

Kwani, mara nyingi, huwa wanatoa kauli za jumla-jumla ambazo zinaweza kutafsiriwa kwa namna nyingi. Pale jambo linapotokea, wao hutafsiri kauli zao kwa namna itakayofanya ionekane ni sawasawa kabisa (kwamba imetokea vilevile kama walivyotabiri).

Kuna nyakati na nyakati huwa wanapatia, hiyo hutokana na jicho la ung’amuzi na ujanja wao wa kulielewa jambo na kulikatia shauri la papo kwa hapo. Kuna nyakati nyingine, hiyo hutokana na majini wanaokutana nao ambao huwapa habari walizoziiba mbinguni.

Katika Sahih mbili na katika Musnad Ahmad, imesimuliwa kutoka kwa Aisha kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehema na amani zimshukie) aliulizwa kuhusu waaguzi. Akasema, “Hawana lolote.”

Wakamuuliza (Mtume), “lakini mbona wakati mwingine huwa wanasema maneno ambayo yanakuwa kweli.” Akajibu, “Maneno hayo ya kweli hutokana na yale aliyoyaiba Jini (mbinguni). Yeye humnong’oneza masikioni jamaa yake (wa kibinaadamu) na huchanganya (ukweli huo) na maneno mia moja ya uwongo.”

Iwapo taarifa wanazozitoa waaguzi kumpa mtu ni sahihi kama vile kulitaja jina la mwizi au kulijua jina la mtu na ndugu zake wa familia kabla ya kukutana nao hata mara moja, basi hilo laweza kuwa limefanyika kwa njia ya ujanja fulani.

Laweza kuwa limefanyika kwa kuwa na msaidizi ambaye hupata taarifa kwa watu au huweza kuyasikia mazungumzo ya wahusika kabla hawajenda kwa mwaguzi. Au yaweza kuwa imetokana na vitimbi vya mashetani kwani mashetani kuyajua mambo yaliyokwishatokea si jambo geni wala la ajabu.


Watabiri ni mitume wa Ibilisi

Ibn al-Qayyim kaandika hivi,

Watazamiaji na watabiri ni mitume wa Ibilisi. Hii ni kwa sababu washirikina ndio wanaowakimbilia watu hao. Wanawakimbilia kwenda kutizamia pale jambo fulani zito linapotokea na huamini maneno yao.

Wanawafanya kuwa waamuzi wa mambo yao na wanaridhia hukumu zao. Hii ni sawa na vile wafuasi wa mitume (wa Mwenyezi Mungu) wanavyokuwa mbele ya mitume.

(Washirikina) huamini kuwa (wapiga ramli hao) wana elimu ya ghaibu. Wanawafahamisha mambo ya ghaibu ambayo hakuna mtu mwingine yeyote anayeyajua.

Hivyo, kwa wale wanaofanya shirki kupitia kwa (watabiri hao), basi watabiri hao huchukua nafasi ya mitume kwao. Kwa kweli, wapiga bao na watabiri ni mitume halisi wa Ibilisi.

Yeye huwatuma kwenye kundi la washirikina na huwafanya waonekane kama mitume wa kweli mpaka kundi lake hilo (kundi la Ibilisi) liwaitikie, ili liwaweke watu hao mbali na mitume wa Mwenyezi Mungu.

Washirikina hao huitakidi kuwa mitume wao ni wakweli na wana elimu ya ghaibu. Kwa vile ipo tofauti kubwa na upo mgongano mkubwa kati ya mitume wa Mwenyezi Mungu na mitume wa Ibilisi, Mtume wa Mwenyezi Mungu kasema, “yeyote anayekwenda kwa mtizamiaji na akaamini kile anachokisema, huyo kakadhibisha kile kilichoteremshwa kwa Muhammad.”

Kwa hiyo, watu wanagawanyika makundi mawili: kuna wafuasi wa watabiri na wafuasi wa mitume (wa kweli wa Mwenyezi Mungu). Hakuna yeyote anayeweza kuwamo katika makundi yote mawili (kwa wakati mmoja).

Kwa hakika, kadri mtu anavyojiweka mbali na Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, ndivyo anavyozidi kuwa jirani zaidi na mtabiri. Na humkadhibisha Mtume kwa kadri anavyomwamini mtabiri.

Yeyote anayesoma historia ya mataifa mbalimbali duniani atatambua kuwa waaguzi na wachawi (waganga) wamepewa hadhi sawa na ile ya mitume. Lakini hawa ni mitume wa Ibilisi. Walikuwa ni watabiri na wachawi (waganga) hawa ambao walisikilizwa na watu.

Wao ndio waliowaamulia kipi halali na kipi haramu. Wakawalia watu fedha. Na wakawaamuru watu kufanya aina nyingine za kaida na ibada ambazo ndizo zilizomfurahisha Shetani. Na wakawafitini watu wavunje undugu na wakavunja heshima za watu. Al-Ahqqad amezungumzia mambo haya katika kitabu chake Ibliis.

Wajibu wa Umma wa Kiislamu kwa Watabiri

Wanachodai wanajimu, watabiri, waganga na waaguzi ni upotoshaji mkubwa ambao haupaswi kuchukuliwa kirahisi-rahisi. Lazima ukataliwe na kukomeshwa.

Ni jukumu la wale ambao Mwenyezi Mungu amewapa dini Yake na kuwafundisha Kitabu Chake na Sunna ya Mtume Wake kuufutilia mbali upotoshaji huo kwa kuusema, na kwa kubainisha uwongo wa madai yao kwa kutoa dalili zilizo wazi.

Na wale wenye uwezo basi watumie uwezo wao huo kuwazuia kwa mkono wale wanaodai kuwa na elimu ya ghaibu, kama vile wapiga ramli, watabiri, wasoma alama za viganja, wasoma vikombe vya chai na kadhalika.

Lazima wazuiwe wasieneze athari zao katika majarida na magazeti. Yeyote anayewatangazia habari zao hadharani lazima aadhibiwe kwa (kusaidia) uovu huo wanaoufanya watu hao. Mwenyezi Mungu aliwalaumu Wana wa Israil kwa kushindwa kuzuia uovu waliouona miongoni mwao,

“Hawakuwa wenye kuzuiana (kukatazana) mambo mabaya waliyokuwa wakiyafanya.” (5:79). Na Mtume amesema, kama alivyosimulia Abu Bakr na kunakiliwa katika Vitabu vya Sunan,

“Kwa hakika, kama watu wanauona uovu na kisha wasiuzuie, basi Mwenyezi Mungu atawasibu kwa msiba mkubwa.”

Kila mmoja wenu ni mchunga na ataulizwa kwa alichokichunga.
Last edit: 3 years 6 months ago by Mfaume.

Please Log in or Create an account to join the conversation.

Time to create page: 0.387 seconds