×
INSHA YA UCHUMAJI KARAFUU (21 Apr 2016)

Assalaam alaykum.
Tunakaribisha insha zinazoelezea shughuli za uchumaji karafuu.

Safari yangu ya Utalii Mikumi kwa Jicho la Tauhidi

More
3 months 2 weeks ago #2790 by
Na Abu Salha
Utalii katika mbuga au hifadhi za wanyamapori na misitu ya uoto wa asili ni moja ya fursa muhimu za kujenga imani na hatimaye yakini kwamba ulimwengu huu una Muumba aliyeyakadiria na kuyaongoza maisha ya viumbe wote.
Qur’an inatuzindua: “Litukuze Jina la Mola wako aliyeumba na Akakitengeneza na Akakikadiria na Akakiongoza (kila kiumbe) na Aliyeotesha malisho.” (87:1-4)
Huenda ulimwengu wetu wa wanadamu hutudanganya pale tunapoitegemea sayansi yetu ya jamii inayotutisha kwamba bila kudhibiti uzazi kwa vidonge, vitanzi na mipira, basi tutakuwa wengi kupita kiasi na hivyo, tutashindwa kujihudumia kwa chakula, maji, na kadhalika.
Mwanadamu amejiundia taasisi kwa msingi wa Sayansi yake ya jamii. Taasisi zake za takwimu zinamtisha na kumtia hofu kwamba idadi ya watu imekuwa kubwa mno katika jamii, hivyo, anahitaji kupunguza uzazi!
Sayansi imemsahaulisha au kumghafilisha kabisa mwanadamu kwamba nje ya jamii yake kuna viumbe lukuki ambavyo maisha yao tangu vilipoumbwa hayategemei sayansi wala taasisi yoyote ya mwanadamu.

Wanyamapori ni mfano hai wa viumbe ambao mfumo wa maisha yao unatosha kumsuta mwanadamu kwamba asijifanye ana akili sana ya kutomuhitajia Muumba katika maisha yake.
Asijitie ujinga wa kuamini kwamba yeye si zao la Kazi ya Muumba, bali ni zao la “nature” iliyompendelea kipawa cha akili baada ya kupitia hatua za unyani na ukima!
Mwanadamu anajaribu kujibaraguza kwamba maisha yake ya sayansi na teknolojia ni zao la akili yake. Kwamba sayansi ndiyo inayojibu matatizo yake, ndiyo inayotibu magonjwa yake, ndiyo inayotafiti na kukadiria mahitaji yake, na kwamba teknolojia ndiyo inayotimiza mahitaji ya sayansi.
Wimbo wake wa Sayansi na Teknolojia unavuma kwa minajili ya kufifiliza ukweli unaothibitika katika maisha ya viumbe vingine kwamba Muumba ndiye Aliyakadiria maisha yake kwa maana ya kumwekea mazao ya chakula, maji, hewa na kadhalika.
Kwa kufanya utalii wa kuyaona maisha ya wanyamapori, mwanadamu mwenye kutumia vema kipawa chake cha kufikiri na mwenye kuzingatia maudhui ya ufunuo, anapata fursa adhimu ya kuimarisha imani yake kwamba ulimwengu katu si zao la bahati nasibu ya maumbile bali ni Kazi maridadi ya Muumba, Mjuzi wa yote na Mwingi wa hikima.
Wazo langu la kufanya Utalii wa Ndani
Wazo la kufanya utalii wa ndani lilinijia wakati nikipanga ratiba yangu ya mapumziko ya mwisho wa wiki katika Juma la Mwisho la Mwezi Agosti. Nikapanga kuchukuzana na familia yangu kwenda Morogoro, Mkoa niliozaliwa.
Moja kwa moja, nikaiongoza familia yangu hadi Mikumi, moja ya hifadhi maarufu za wanyamapori nchini. Licha ya kuzaliwa na kuishi Morogoro kwa miaka mingi ya utoto wangu, sikupata kutembelea Mikumi hata siku moja.
Hii ni mara yangu ya kwanza kufika kwenye kijiji cha Mikumi ambacho jina lake limepata umaarufu wa kimataifa kwa sababu ya hifadhi ya wanyamapori.
Nilipendelea zaidi kusafiri na Noah kwa kuamini kuwa ingefaa zaidi kule mbugani kwani ina bodi gumu. Sikujua kuwa kumbe kule Mbugani kuna magari maalum ya utalii.
Tukatoka na Noah yetu Jijini D’salaam majira ya asubuhi. Barabara zetu za kuunganisha mikoa sasa ni nzuri,mkeka mtupu hadi Mikumi. Kwa mwendo wa wastani bila kuchokoza tochi za askari wa usalama barabarani, tulifika Morogoro mjini milango ya adhuhuri.
Ilituchukua takriban saa mbili kusafiri kutoka Moro mjini hadi Mikumi. Mikumi inatanguliwa na kijiji cha jirani cha Doma. Japo Doma iko nje ya Hifadhi lakini wakazi wake hawaishi kulalamikia uvamizi wa wanyamapori katika mashamba yao.
Tembo na wanyama wengine hushambulia mazao yao mara kwa mara. Wanakijiji hawa wanalalamika kwamba hawana la kufanya kwani kuwadhuru wanyama hao ni hatia ambayo hukumu yake ya kisheria ni kali.
Kwa wageni kama sie,kusimuliwa mikasa hiyo ya kuvamiwa na wanyama kungetosha kutufikisha katika hitimisho kuwa Doma si mahala salama pa kuishi, na tusithubutu kulala mahali pa kutisha namna hiyo!
Hadithi ya kuvamiwa na tembo, mnyama mkubwa kuliko hata vibanda vya wanakijiji, ingetukosesha au kutunyima usingizi usiku kucha kama tungelazimika kulala Doma!
Lakini kwa wanaDoma, hayo ni maisha ya kawaida. Doma ni kijiji kikongwe ambacho ni vigumu kusema kama kimo ndani ya hifadhi. Ni vigumu kujibu swali la nani wa kulaumiwa kati ya binadamu wanaoishi Doma na wanyama wanaovamia kijiji hicho mara kwa mara.
Kwa mie mpita njia, wazo lililonijia ni kwamba kama kimo ndani ya hifadhi au jirani na hifadhi basi wanakijiji wangepewa fidia ya kutosha kuhamisha makazi yao badala ya kuishi kwa misukosuko na hasara ya mali na hata maafa.
Lakini hilo ni wazo la mpita njia. Wenyewe wenyeji wameshazoea kuishi hivyo. Wamezaliwa na kukulia hapo. Kuwahamisha huenda kukawa sawa na kuifuta historia yao tangu enzi za mababu zao waliozikwa hapo.
Ipo haja kwa serikali kuwafikiria wakazi hawa wa Doma ili wasijione kwamba thamani yao ni ndogo kuliko wanyama kwani wanasema wanyama wanapoumizwa, serikali huja juu na kuwasumbua lakini wanyama wanapoumiza hakuna hatua yoyote ya maana inayochukuliwa!
Tunaiacha Doma na malalamiko yake, tunaingia Mikumi. Safari yetu inafika kituo cha mwisho. Barabara kabisa, kwetu, huu haukuwa tu utalii wa ndani ambao kila Mtanzania mwenye wasaa anaweza kuuendea bali lilikuwa ni shamba-darasa kwa mtazamo wa kiimani.
Maisha ya wanyamapori ni somo tosha kwa yeyote anayetaka kuyakinisha theolojia ya kumwamini na kumtukuza Mungu. Kila jamii ya wanyama imepata makazi bora yenye chakula na maji ya kuifanya iishi.
Ikumbukwe wanyama walitutangulia kuumbwa muda mrefu kabla baba yetu Adam hajateremshwa duniani. Waliishi kama tunavyowaona leo bila usimamizi wetu.
Wanyama wanaokula nyama walikuwepo, na wanaokula nyasi na majani walikuwepo. Wanyama wa magondi walikuwepo na wanyama wa kutambaa (watambazi) walikuwepo.
Ndege walikuwepo na wadudu walikuwepo. Jamii hizi za viumbe hazikuhitaji mamlaka za hifadhi ya wanyamapori wala askari wa hifadhi. Wanyama waliishi wenyewe kwa kipindi kisichokadirika au tuseme miaka dahari kabla ya mtu wa kwanza kuja duniani.
Elimu ya viumbe anayosoma mwanadamu ni matokeo ya kuzitafiti jamii za wanyama. Sio mwanadamu aliyewafunza wanyama kuishi wanavyoishi. Wanaishi maisha asilia ambayo ng’ombe wetu wa maziwa wanaoishi kwa kutegemea kemikali za madawa na vyakula vya kutengenezwa viwandani wameyapoteza.
Ukila nyama pori, umekula nyama salama inayokubalika moja kwa moja kwenye mtambo wa mwili unaojumuisha mfumo wa damu wenye vimeng’enya vya kuchakata chakula na kusambaza virutubisho katika sehemu mbalimbali.
Malalamiko juu ya hali tete za afya zetu zinazojumuisha magonjwa ya mishituko ya moyo, mapigo-kasi ya moyo, viharusi, saratani na kadhalika ni matokeo machungu ya mkono wa mwanadamu uliochakachua mfumo wa ulaji na uzalishaji wa wanyama wetu wa kufugwa majumbani.
Nyati ameumbwa na hasira kali ili kuuhami mfumo wake wa maisha. Kwa sababu ya kutoguswa na mkono wa mtu, nyama yake, bila shaka na maziwa yake yamebaki salama kwa afya ya mwanadamu. Bora wanyama hawa waendelee kujikalia hukohuko porini ili kuepuka maabara za uharibifu au ufisadi.
Tukiwa ndani ya Gari maalum ya utalii ya kutokezesha vichwa juu, tunawaona simba. Ni wanyama hatari kuwakaribia. Askari-mpagazi akaokota jiwe na kuwashitua.
Wakainua vichwa kuangalia kilichorushwa. Ujazo wa misuli yao unampa kila mtalii ishara kuwa ni wanyama wenye nguvu sana. Macho yanakukubalisha kuwa ni kazi ngumu kupambana na mnyama huyu.
Nikakumbuka kisa cha babu yangu, mjomba wa baba yangu, aliyepambana na samba katika eneo ambalo sasa limejengwa mabweni wanayoishi wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine, SUA.
Ni upande wa kulia wa geti la kuingilia SUA. Mapambano yalikuwa makali lakini kwa nusura ya Mungu, akatokea nguruwepori, Simba akaachana na babu yangu na kumkimbiza nguruwepori.
Babu alilazwa hospitalini miezi sita. Enzi hizo eneo husika lilikuwa pori tupu, tofauti na linavyoonekana leo ambapo barabara ya lami, majengo na watu wamelifanya liwe mji.
Kwa mtu anayemtazama simba kwa jicho la tafakuri juu ya Muumba anaona kirahisi kwamba mfumo wa ulaji wa mnyama huyu umehitaji awe na nguvu, maarifa ya kuwinda, kucha kali na mbio.
Angekosa sifa hizi, mnyama huyu angekufa njaa siku nyingi kabla ya binadamu kuja duniani. Simba anahitaji nguvu kukamata mnyama kama nyati, anahitaji maarifa ya kumvizia ili asije kufa yeye!
Anahitaji mbio za kumfukuza Swala! Na anahitaji kucha za kuwararuria. Maisha haya ya mnyama asiye na akili haiingii akilini kuwa yamejipanga yenyewe kwa kile kinachoitwa “nature”.
“Nature” isiyofafanulika haingeweza kuyakadiria maisha ya Simba kwa usahihi namna hiyo ambapo simba kwa mfumo wao wa maisha ya kuwinda wanyama wengine, wameendelea kuishi hadi leo. Sifa pekee za kuwinda za samba nazo pia zisingekuwa na maana kwa maisha yake kama kusingelikuwa na wanyama wa kuwindwa.
Ndani ya gari yetu ya utalii, tunaona makundi ya nyati. Tukaambiwa hao ni nyati waliohamia Mikumi kutoka mbuga nyingine. Ni nyati mia nne. Hawa ni wanyama wanaokula nyasi.
Maisha yao yanategemea uoto endelevu wa nyasi. Laiti majani yangekauka siku nyingi kabla ya binadamu kuja duniani, basi asingewakuta wanyama hawa.
Nyati wameishi maisha ya uhakika kwa sababu ya uoto wa kudumu wa nyasi. Ni rahisi kukubali kuwa Aliyemkadiria Nyati maisha yake ya kula nyasi Ndiye Aliyeotesha nyati kwa mfumo wa uoto wa kudumu.
Binadamu kazusha kilio cha kutoweka kwa mimea na miti ya uoto wa asili baada ya kufanya uharibifu. Ni yeye aliyeiharibu ekolojia, kisha anasingizia “mabadiliko ya tabia ya nchi.”
Jicho la tafakuri juu ya Muumba linampa mtu uhakika kuwa sio “nature” bali Mungu Muumba ndiye aliyekadiria maisha ya nyati na kumuongoza kuishi anavyoishi.
Ndani ya gari la utalii, tunaona tembo, wanyama wakubwa ambao nguvu zao zinawazidi wanyama wote. Tukaambiwa hawa ni wanyama wanaoishi kifamilia. Kila kundi linajumuisha tembo wa familia mahususi.
Chakula cha tembo ni majani. Kama wanyama wengine walao nyasi, tembo wamehakikishiwa usalama wa chakula tangia zama na zama kabla ya kuumbwa binadamu. Uoto endelevu wa asili wa majani na nyasi umewawezesha wanyama hawa kuishi hadi leo.
Ndani ya gari la utalii, tunaona mabwawa ya maji. Mabwawa haya yanayowahakikishia maji wanyama yalikuwepo karne nyingi kabla mwanadamu hajaunda vijiko vya kuchimbia ardhi.
Hayakuwekwa na Wizara ya Maliasili wala mamlaka za hifadhi. Wanyama wote wa kunyanyuka na wa kutambaa wanakunywa maji ya kuwahakikishia uhai wao katika mabwawa hayo. Tukaambiwa katika moja ya mabwawa, mna joka kubwa sana, ni hatari kulikaribia.
Kwa hakika tumeburudika na kujifunza katika safari yetu ya utalii Mikumi.
Maoni tuma 0688900900

Please Log in or Create an account to join the conversation.

Time to create page: 0.491 seconds