×
INSHA YA UCHUMAJI KARAFUU (21 Apr 2016)

Assalaam alaykum.
Tunakaribisha insha zinazoelezea shughuli za uchumaji karafuu.

Watoa khutba za Ijumaa waielewe hadhira yao kabla ya kupanda juu ya mimbari

More
11 months 22 hours ago #2712 by
Azadi Mpango
Kila siku ya Ijumaa Misikiti mingi nchini na ulimwenguni kwa ujumla hurindima khutba. Hili hutokea kabla ya kuswali rakaa mbili kwa ajili ya Swala ya Ijumaa inayochukua nafasi ya swala ya Adhuhuri katika siku nyingine za kawaida.

Khutba ya Ijumaa inahudhurishwa mbele ya ummah uliohudhuria Misikitini. Mtoa au msoma khutba ya Ijumaa ambaye hujulikana kwa lugha ya Kiarabu kama ‘khatibu,’ husimama mbele ya kadamnasi ya Waislamu na kusema kile alichoandaa ili kiwe ujumbe wa juma zima.

Huwa ni ujumbe unaotakiwa sio tu kuachwa mara baada ya kukimiwa swala au kutoka nje ya Misikiti. Sio waadhi au burudani ya kukamilisha ratiba kwa sababu imepaswa kuwepo kama mafundisho ya Uislamu yanavyoelekeza.

Bali inapaswa kuendelea kuwa mithili ya mwangwi unaosumbua ngoma za masikio ya Waislamu waliopata wasaa wa kusikiliza khutba kwenye Misikiti mbalimbali kwa masiku yote yanayofuata mpaka pale watakapokutana na Ijumaa nyingine yenye ujumbe mwingine.

Lakini hilo la kulibeba na hatimaye kulifanyia kazi ndani ya takribani siku sita na pengine maishani halitawezekana iwapo ujumbe wenyewe haujaeleweka ipasavyo. Ni muhali kuondoka na jambo ambalo halina kichwa wala miguu na kwa maana hiyo waandaji wawe makini.

Kwamba ‘makhatibu’ kwenye Misikiti yote ni vyema watambue kama sio kujifunza mbinu mbalimbali za kuwasilisha ujumbe mbele ya watu wenye vipawa tofauti vya kuelewa na kunasa. Ni vyema wakaumiza vichwa vyao kufikiri ujumbe utakaofaa kutolewa ili ubaki ndani ya wiki nzima.

Hiyo ni kazi ngumu, lakini hainabudi kuhangaikiwa ili lipatikane suluhisho ambalo bila ya shaka litasaidia kuukimbiza usingizi wa ghafla wa Waislamu unaowakumba katika kipindi ambacho khutba ya Ijumaa huwa ikiendelea.

Itasaidia kupunguza kama sio kumaliza moja kwa moja uchelewaji wa makusudi wa Waislamu wengi wanaokimbilia kupata rakaa mbili tu za Ijumaa badala kuanza kuwahi kusikiliza khutba mbili za Ijumaa na hatimaye kuondoka na ujumbe wa juma zima.

Huu ndio ukweli usiopingika kwamba karibu asilimia kubwa ya Waislamu wamebeba moja wapo kati ya tabia hizi mbili, yaani kulala wakati wa khutba au kuichelewa kabisa. Lakini kwa upande mwingine wa shilingi ni kuwa ‘makhatibu’ nao wanachangia haya kwa njia moja au nyingine.

Huenda na wao hawajui kwamba ni moja ya chanzo cha Waislamu wengi kuondoka Misikitini mara baada ya swala ya Ijumaa wakiwa hawana lolote kuhusu kilichoongelewa. Hawana ujumbe wa kuufanyiakazi wala kuwapelekea wengine ambao hawakubahatika kusikia khutba ya juma husika.

Watapeleka nini wakati wao wenyewe walilala au walichelewa kipindi cha khutba na tangu hapo hata hiyo khutba yenyewe nayo haieleweki? Muhali huu unaweza kumalizwa na ‘makhatibu’ wetu wa Ijumaa kwa kujua mbinu nzuri za kuwasilisha.

Kwamba kile kitendo cha kutambua tu njia hasa bora za kufikisha mbele ya watu itabadili khutba za Ijumaa zilizojaa mazowea yanayoendelea kuwashawishi Waislamu kusubiri muda halisi wa kupata rakaa mbili za Ijumaa pasi na kujali kuwa kabla yake pana khutba ambayo nayo inawahusu wao.

Ni lazima ‘makhatibu’ wachague mada (ujumbe) zinazogonga wakati uliopo huku wakijaribu kuzama ndani zaidi ili kuwapa muamko wasikilizaji. Mwanzo wa mada iwapo utakuwa mzuri ndivyo utakavyoshawishi wasikilizaji huku kinyume chake kutawapelekea wawaze khutba bora iishe.

Uchaguzi wa mada uendane sambamba na uchaguzi wa lugha. Kwamba wakati mwingine lugha isiyoeleweka hupelekea kuharibu mada nzima kiasi cha kufanya hata lengo ambalo ni kupatikana kwa ujumbe wa juma kutofikiwa.

‘Makhatibu’ ni vyema wakawa makini na matumizi ya lugha. Hata kama khutba inatakiwa iwasilishwe kwa lugha ya Kiarabu mathalani, basi ni vyema kikatumika cha kawaida (simple Arabic) badala ya kuchagua ‘mabombastiki’ yanayotaka kufungua kamusi jambo ambalo ni muhali.

Na kwa kuwa Misikiti mingi hapa nchini hutumia lugha ya Kiarabu pamoja na Kiswahili, basi ni aula kwa ‘makhatibu kuona umuhimu wa kutumia zaidi lugha inayoeleweka na wengi ili kuwepesisha kueleweka kwa kilichokusudiwa.

Yote kwa yote ni kwamba lugha itakayotumika isiwe ngumu (complex language) kwa wasikilizaji wa khutba ya Ijumaa. Kusiwe na mchanganyiko wa lugha kiasi cha kuwachanganya wafuatiliaji na pia ni vyema ikatumika mifano hai iliyopo kwenye jamii wakati ‘khatibu’ akisherehesha mada yake.

Katika hali ya kawaida inapendeza kwa mhutubu kutotumia muda mrefu kuzungumza kutokana na ukweli kuwa wengi wetu sio tu wamebanwa na shughuli bali hawana mazowea ya kukaa kitako kusikiliza jambo kwa kitambo kirefu, hivyo ni bora kufupisha khutba.

Sio mwiko kurudia rudia kusikopitiliza kwa baadhi ya nukta muhimu kama vile anuani ya khutba pamoja na lengo au malengo yake ili kuwakumbusha wasikilizaji pamoja na kuwaleta karibu wachelewaji ambao miongoni mwao huchelewa kwa dharura.

Iwapo ‘makhatibu’ wa Ijumaa wakiielewa vyema hadhira yao, hawatapata tabu wao binafsi lakini itasaidia sana ujumbe wa siku ya Ijumaa ukafika vilivyo na kinyume chake itakuwa ni kuliacha kundi kubwa la Waislamu likitoka kapa Misikitini bila ya kujua kilichosemwa wakisubiri rakaa mbili tena juma lijalo.

Pia ni vyema ‘makhatibu’ wakakumbuka kuwa mimbari za Ijumaa sio mahali pa kulipiana visasi kwa kusemana kutokana na tofauti za kimakundi, kitaasisi au maslahi yoyote yale na badala yake waitumie kama ilivyokusudiwa kuwa ni mahali pa kufikishia ujumbe wa juma mbele ya jumuiko la Waislamu.

Kumbukumbu hii itasaidia kutafuta ujumbe usioleta msuguano wowote ambao huenda ikawa chanzo cha kuwatoa umakini baadhi ya wasikilizaji wa khutba ya Ijumaa. Aidha maendeleo ya kiteknolojia nayo yanaweza kutumika ikibidi ili kusambaza ujumbe wa Ijumaa uliotolewa kwenye Misikiti tofauti.

Na kwa Waislamu nao ni vyema wakawahi Misikitini siku ya Ijumaa mapema kadiri ya uwezo wao na wahakikishe wanakuwa hadhiri kwa ajili ya kusikiliza na kuelewa vyema ‘khutba’ za Ijumaa zinazowasilishwa mbele yao.

Kwa maoni, tuma SMS: 0714 789 265.

Ukinyoa upara usiokote madoriani

Please Log in or Create an account to join the conversation.

Time to create page: 0.412 seconds